Nani anamchukia Fiston Mayele na kwanini?

IMESHANGAZA kidogo. Fiston Kalala Mayele ameandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram akilalamika kwamba kuna mashabiki kutoka Tanzania wamekuwa wakimchukia. Akaenda mbali kwa kudai kwamba hata viongozi wamekuwa wakimchukia.

Alipochokonolewa zaidi Mayele amedai kwamba yeye sio Mtanzania. Nadhani alikuwa anataka kutupa ujumbe kwamba alikuja nchini kutafuta maisha na sasa ameondoka. Kwamba hakuna haja ya chuki dhidi yake.

Maswali mawili ya msingi. Nani anamchukia Mayele Yanga? Tuanzie kwa viongozi. Inatajwa kwamba Mayele alipambana sana katika kuondoka kwake kwa sababu Yanga walikuwa wamepania kumbakiza. Anahisi kwamba viongozi walikuwa wanataka kumharibia maisha.


Kwa mtazamo wangu, kama kuna mabosi wa Yanga walikuwa wanataka kumfanyia mtimanyongo Mayele asiondoke na kwenda Misri kupata mshahara mkubwa, basi hapo walifanya roho mbaya. Kama walikuwa wanapambana kumzuia kwa kumuahidi kumlipa vizuri basi hiyo haikuwa nia mbaya. Lilikuwa jambo la kawaida katika soka.

Hilo la pili ni jambo la kawaida tu hata katika kazi zetu za kawaida. Unafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, unapata ofa kwingineko, mabosi wako wanapambana kukuzuia kwa kukuahidi mshahara mkubwa na marupurupu mengine.

Inanishangaza kama baada ya mabosi wa Yanga kushindwa kumbakiza Mayele kuliingia chuki ndani yake. Chuki ya nini? Siwezi kuelewa. Yanga washukuru kwamba Mayele hakuondoka bure na walipata kiasi kikubwa cha pesa baada ya mauzo yake kwenda Pyramids. Ilikuwa ni biashara.


Hata kama ilikuwa ni biashara ambayo ilifanyika kwa kinyongo lakini walipata pesa. Na hapo hapo ni wazi kwamba hata wenyewe walifahamu kwamba mshahara ambao Mafarao walikuwa wamemuahidi Mayele ulikuwa maji marefu kwao.

Tukigeukia upande wa mashabiki wa kawaida hapa ndipo ninapomshangaa Mayele. Kwanini anapenda kujibizana na mashabiki katika mitandao? Ni kweli huenda kuna mashabiki wa Yanga wanamsemesha vibaya mitandaoni na hilo ni jambo la kawaida tu katika mpira.

Wakati mwingine kibinadamu kuna kundi la mashabiki wa Yanga ambao bado wameumizwa kuondoka kwa Mayele. Mashabiki wengine huwa wana ufahamu mdogo katika mchezo wenyewe. Hawajui kwamba mchezo wenyewe umekuwa biashara kubwa siku hizi.


Mashabiki siku zote huwa wanaamini kwamba wachezaji wana mapenzi na timu zao kama wao. Kisa? Wakifunga huwa wanashangilia nao. Hapana. Mchezaji kama Mayele amesema kweli. Ameweka wazi kwamba yeye alitoka DR Congo kuja nchini kutafuta maisha.

Tatizo la Mayele ni majivuno fulani ambayo anayo. Anafahamu kwamba kauli yake itazua taharuki nchini kwa sababu yeye bado maarufu hapa nchini. Angeweza kukaa kimya tu na kufanya mipango yake kuliko kujali sana masuala ya mitandao ya kijamii. Haimsaidii.

Wachezaji wa kulipwa kazi yao ni kucheza soka na kupuuza kelele za mashabiki. Mashabiki kazi yao kubwa pia ni kukutoa mchezoni. Kukabiliana na changamoto za wachezaji wa timu pinzani na pia mashabiki wa timu pinzani pamoja na wale mashabiki wako ni kazi ya mwanasoka wa kulipwa.

Mifano ipo mingi na hasa kwa mfano huu wa mchezaji kushambuliwa na mashabiki wa timu yako. Mifano mizuri inapatikana katika klabu ya Simba. Majuzi hapa baada ya kusimamishwa na uongozi wa klabu ya Simba, kiungo Clatous Chama alikuwa akishambuliwa na mashabiki wa timu yake pindi alipojitokeza katika mitandao ya kijamii.

Mpaka leo Chama hajawahi kujibizana na mashabiki au kutangaza chuki ambayo inamzunguka kutoka kwa baadhi ya mashabiki au viongozi wa klabu ya Simba. Ni vivyo hivyo kwa wachezaji kama Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.


Majuzi tu hawa mastaa walikuwa wakilalamikiwa na mashabiki wao kwamba wamechoka na wamezeeka. Kwamba hawana tena uwezo wa kuipeleka timu mbele. Uliwahi kuona wanajibizana na mashabiki katika mitandao ya kijamii?

Chuki ni sehemu ya maisha ya mchezo wa soka. Kwa Mayele, chuki ni ishara tu ya wivu fulani unaojengeka baada ya kufanya mambo makubwa katika klabu yake hiyo ambayo aliipeleka hadi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama kweli kuna watu wa Yanga wamejenga chuki kwa Mayele, basi tangu naufahamu huu mchezo hapa nchini hii inaweza kuwa mara ya pili kwa watu wa Yanga kumchukia mchezaji ambaye hajahamia kwa watani zao, Simba.

Mchezaji wa kwanza anaweza kuwa Fei Toto alipokwenda Azam. Unaweza kuelewa hasira za mashabiki wa Yanga kutokana na namna ambavyo Fei aliondoka Yanga. Mazingira yalikuwa ya chuki baada ya Fei kuzungumza mambo mengi kiasi cha kesi yake kwenda mbali.

Nyingine inaweza kuwa hii ya Mayele kama kweli anasema kweli. Mbona Mrisho Ngassa aliwahi kuihama Yanga wakati inamhitaji akahamia Azam, lakini Yanga walielewa? Dau ambalo Azam waliweka mezani lilikuwa kubwa.

Mara zote mashabiki na viongozi wanakuwa na chuki dhidi ya mchezaji ambaye amekatiza na kwenda zake Msimbazi. Hata upande wa pili nao wanakuwa na chuki hiyo hiyo kama kuna mchezaji amekatiza na kwenda zake Jangwani. Ni kitu cha kawaida. Hata Ulaya hii chuki inakuwepo.


Mayele angepiga kimya. Angeendelea na mambo yake. Tatizo kubwa lililopo kuanzia wachezaji wazawa hadi hawa wa kigeni wanaokuja nchini ni kurithishwa tabia ya kupenda mitandao. Kama Mayele anachukua simu yake na kutazama mambo mbalimbali yanayoendelea duniani nadhani asilimia tisini ya mambo hayo ni kile kinachoendelea Tanzania.

Watanzania ni hodari katika matumizi ya mitandao kwa namna ya kukashifiana, kukejeliana na mengineyo. Unapokuwa staa tazamia kwamba sio kila mtu atakupenda na kukuzungumzia vizuri. Mayele agekaa kimya tu.

Kuelekea pambano la Pyramids na Mamelodi pale Afrika Kusini, Mayele alikuwa amenyimwa viza ya kuingia Afrika Kusini. Akaenda katika mtandao wake na kuandika kwamba huo ulikuwa mpango tu wa Mamelodi kuhakikisha hachezi pambano hilo. Kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena akamjibu Mayele aachane na mambo ya mitandao.