Namungo tatizo straika

KOCHA Mkuu wa Namungo, Cedric Kaze amesema changamoto ya kukosa straika halisi katika mchezo uliopita ilichangia kushindwa kutumia nafasi nyingi ilizopata na kuinyima ushindi dhidi ya JKT Tanzania.

Namungo ilianza vibaya Ligi Kuu Bara kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa timu iliyorejea katika ligi hiyo.

Kaze alisema: “Tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi, lakini hatukutumia vizuri na niseme tulikuwa na changamoto katika upande wa ushambuliaji kwani hatukuwa na mshambuliaji halisi wa kati. Wachezaji tunaowatumia katika nafasi hiyo, Reliants Lusajo ameumia na hajacheza muda mrefu, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ naye amejiunga na timu na kuanza mazoezi kwa kuchelewa.”

Hii ni mara ya pili mfululizo Namungo inaanza bila ushindi katika mechi ya kwanza ya ligi kwani msimu uliopita ilifungua pazia la ligi kwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar.

Namungo itashuka tena uwanjani wikiendi hii kuikabili KMC kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi.