Nafasi za Simba, Yanga CAF ni hapa

Muktasari:

  • Simba itakuwa ugenini nchini Botswana ikicheza na Jwaneng Galaxy saa 10:00 jioni katika uwanja Francistonw  (kundi B)huku Yanga ikiikaribisha Al Ahly katika uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku.

Klabu za Tanzania kesho zitaendelea kusaka nafasi ya kukaa sehemu nzuri kwenye makundi yao kwa kucheza mechi za pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Simba itakuwa ugenini nchini Botswana ikicheza na Jwaneng Galaxy saa 10:00 jioni katika uwanja Francistonw  (kundi B)huku Yanga ikiikaribisha Al Ahly katika uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku.

Timu zote hizo huu ni mchezo muhimu kwao kwani Simba ina pointi moja baada ya kutoka sare ya 1-1 na Asec Mimosas hivyo inahitaji ushindi ili kupata pointi nne na kukaa sehemu nzuri kwenye msimamo wa kundi lao.

Kundi la Simba kinara wao ni Galaxy ikiwa na pointi tatu baada ya kumfunga Wyadad AC 1-0, hivyo bado uwanja upo wazi kwa Simba, Asec Mimosas zenye pointi moja na hata Wydad ambayo haina pointi.

Simba ikipata pointi tatu inakuwa na pointi nne na kuishusha Galaxy huku ikiombea matokeo mabaya mchezo wa ASEC dhidi ya Wydad AC utachezwa siku hiyo hiyo saa 4:00 usiku.

Rekodi ya Simba dhidi ya Galaxy inawabeba  baada ya mara ya mwisho (2017) ikiwa nchini Botswana iliichapa timu hiyo 2-0 lakini katika uwanja wa Mkapa, Simba ilifungwa 3-1.

Upande wa Yanga yenyewe inashika mkia baada ya kufungwa 3-0 na CR Belouizdad lakini faida kubwa ni Medeama nayo ilifungwa 3-0 na Al Ahly.

Yanga kwenye mchezo wa kesho inahitaji ushindi kwani itakuwa na pointi tatu muhimu ambazo itawaweka sehemu nzuri katika kundi D kisha inabidi iombee matokeo mabaya kati ya Medeama dhidi ya CR Belouizdad.

Ushindi wa Yanga utapunguza spidi ya Al Ahly katika kundi hilo hali ambayo itakua ahueni katika kufufua matumaini ya kusaka tiketi ya kucheza robo fainali.

Rekodi inaonyesha wazi Al Ahly mara ya mwisho kucheza kwa Mkapa dhidi ya Yanga ilifungwa bao 1-0 ambalo  lilifungwa na aliyekuwa nahodha wao, Nadir Haroub 'Canavaro'.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alikaa na wachezaji wake na kuanza kuwatengeneza kisaikokolojia kuhakikisha wanakuwa sawa ili kuweza kucheza mchezo huo.

Benchikha aliwataka mastaa wake akili zao ziwe sawa na kusahau matokeo ya nyuma na sasa wafikilie zaidi mchezo huo huku akikisisitiza mchezaji yeyote ana nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake.

"Hakuna jina au mtu ambaye ana uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza badala yake kila mmoja ana nafasi, yule atakayeonyesha kiwango kizuri mazoezini ndiye atakayepata nafasi ya kucheza,"alisema Benchikha.

Upande wa kocha wa Yanga, Miguel Gamond aliliambia gazeti mama na hili (Mwanaspoti) kwamba mchezo uliopita ulikuwa darasa na hawataki kurudia tena makosa.

"Kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika kwa wachezaji wangu ili tuweze kupata matokeo katika mchezo huu na litafanikiwa kwa sababu ni maelekezo ya kiufundi;

"Malengo yetu ni kusonga hatua inayofuata na hilo linawezekana kama wachezaji wangu watacheza kwa malengo  na ushindani."