Nado, Lyanga watajwa Simba

Tuesday June 22 2021
pic nado
By Thomas Ng'itu

KOCHA wa viungo Simba, Adel Zrane ameshindwa kujizuia juu ya mawinga wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’ na Ayoub Lyanga kuingia kwenye rada za moja ya timu moja ya Tunisia.

Adel ni kocha anayetoka nchini humo, aliwasifia wachezaji hao wa matajiri hao wa Bongo wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na wapinzani wao wa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Kocha huyo alisema alipigiwa simu na mmoja wa mawakala wakubwa kutoka Tunisia na aliwaulizia juu ya Nado na Lyanga lakini alimuambia ni wachezaji wazuri na wapo kwenye timu ya taifa Tanzania, (Taifa Stars) ilipokuwa ikijiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi.

“Nadhani atakuwa ameshawasiliana na wahusika. Niseme kweli, ni wachezaji wazuri wana spidi, mimi binafsi nimekuwa nikiwafuatilia,” alisema Adel.

Juu ya nyota wa kikosi chake, Adel alisema karibu wote wanaweza kwenda kucheza sehemu yoyote ile kutokana na utayari wa kimwili na kiuchezaji ambao tayari wanao mpaka sasa.

“Wachezaji wa Simba kwa sasa wanacheza kokote, wapo vizuri katika kila idara na wanaweza kushindana na ikitokea kama mmoja wapo anaenda nje basi anaweza kucheza, ilitokea ile dili ya Manula kama angeenda pia angeweza kucheza,” alisema Adel.

Advertisement

Licha ya Adel kuyasema kuhusu wachezaji Nado na Lyanga, mabosi wa Azam waliwaongezea mkataba wa miaka miwili miwili kuendelea kusalia katika kikosi chao licha ya mikataba yao ya awali kutomalizika. Tetesi za awali Yanga walikuwa wakimpigia hesabu Nado ili awe mbadala wa Tuisila Kisinda.

Hadi sasa, nyota hao wawili wamefunga jumla ya mabao 16, Nado akiwa na 10, akishika nafasi ya pili kikosini nyuma ya Prince Dube, huku Lyanga akifunga sita kati ya mabao 48 iliyofunga timu yao katika michezo 31 ya Ligi Kuu Bara.

Advertisement