Nabi: Tutaelewana tu!

Friday October 01 2021
yanga pic
By Charity James
By Khatimu Naheka

KIKOSI cha Yanga tayari kimerejea jijini Dar es Salaam fasta jana hiyo hiyo kikaingia kambini kwa ajili ya mechi yao ya kesho dhidi ya Geita Gold katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, huku Kocha Nasreddine Nabi akiwatia hasira mastraika wake, Fiston Mayele, Heritier Makambo na Yacouba Songne akitaka wafunge zaidi, huku akifichua kilichofanya wachezaji wake watepete kipindi cha pili kwenye pambano hilo waliloshinda kwa bao 1-0.

Yanga ilikuwa Kagera kwa pambano lao la kwanza la Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na kuondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0, kwenye mchezo mkali uliopigwa Uwanja wa Kaitaba.bao likiwekwa kimiani na kiungo Feisal Salum.

Licha ya ushindi huo, Kocha Nabi alisema hakufurahishwa na nafasi zilizopotezwa na vijana wake na kutaka wajipange zaidi ili kufunga kadri wanavyopata nafasi kwenye mechi zao zijazo.

Yanga haijabeba taji la Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo tangu watani wao, 2017-2018 walipowavua walipokuwa wakikishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

Kwa msimu huu timu hiyo imeonyesha ni ya kurejesha heshima, kwani imeanza kubeba Ngao ya Jamii ikiifunga Simba katika mechi iliyopigwa wiki iliyopita.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo, Nabi alisema kukosa umakini kwa washambuliaji wake ndio kulikowapa mchezo mgumu kipindi cha pili, wenyeji waliporudi na moto.

Advertisement

Nabi alisema walikuwa na nafasi ya kumaliza mchezo bila presha kipindi cha kwanza kama nyota wake wangetumia nafasi walizopata na kusema atazungumza nao ili kuvuna mabao mengi yatakayowafanya wasiwe na presha mchezoni kama ilivyokuwa juzi.

Katika mchezo huo wa juzi Kocha Nabi alianza na mshambuliaji mmoja wa kati Mayele akisaidiana na Feisal Salum, Yacouba, Farid Mussa na Jesus Moloko kabla ya kipindi cha pili kuwatoa kisha kuwaingiza Ditram Nchimbi, Makambo na Deus Kaseke.

“Wapinzani wetu walirudi kipindi cha pili na nguvu mpya na kutushambulia a kukaba mianya waliyokuwa wanapita wachezaji wangu mwanzoni, nadhani tutabadilika kwa mechi zijazo.”

Hata hivyo, Nabi alifafanua sababu ya vijana wake kupoteza umakini akisema ilichangiwa na nguvu kubwa waliyotumia dhidi ya Simba.

Nabi aliongeza pia kutumia kwao uwanja wa nyasi za bandia kwa mara ya kwanza msimu huu iliwaongezea ugumu wachezaji wake.

“Sio kwamba timu haina pumzi unawezaje kuwa na pumzi ndogo ukashinda kwa nguvu katika mechi kubwa kama ya Simba? Inawezekana watu hawajajua kilichotupa shida,” alisema Nabi na kuongeza;

“Pia tangu tuanze maandalizi ya msimu hatujawahi kutumia uwanja wa nyasi za bandia, unapokuwa na mchoko na kucheza katika uwanja kama ule lazima utachoka zaidi.”


MSIKIE BARAZA

Kocha Mkuu wa Kagera, Francis Baraza alikiri ubora wa nyota wa Yanga, Khalid Aucho, Fei Toto na Yannick Bangala ndio uliowanyima ushindi nyumbani na kudai kama Yanga itaendelea na moto huu itasumbua sana msimu huu.

“Namfahamu vizuri sana Aucho tangu tupo Kenya amecheza Gor Mahia na Tusker nimemshuhudia kabla ya mchezo nilizungumza na wachezaji wangu kuhakikisha wanamkaba, lakini kwa ubora na uzoefu alitumia mbinu nyingine kuwakwepa kwa kupanda juu kidogo,” alisema Baraza.

“Ubora wa nyota hao pamoja na Mukoko kama watawatumia mizuri Yanga watakuwa na msimu bora,” alisema Mkenya huyo.

Advertisement