Mziki wa Arsenal kuuzima ujipange kweli

Muktasari:

Msimu huu, kocha Unai Emery anakwenda kuwatesa wapinzani wake na bunduki hizo, huku akiziongezea nguvu zaidi kwa kumleta kiungo mpishi, Dani Ceballos na winga matata, Nicolas Pepe. Kocha Emery ameboresha pia kwenye safu yake ya ulinzi, akimleta David Luiz kufunga duka kabisa.

LONDON, ENGLAND. Arsenal pointi sita tayari kibindoni. Mambo safi kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Staa straika wa kikosi hicho, Alexandre Lacazette wamewachimba mikwara wapinzani, akiwaona: “Haya mnayaona ni mambo yangu mazuri tu, bado yale bora."
Straika huyo Mfaransa aliweka nyavuni kwenye ule ushindi wa 2-1 iliyopata dhidi ya Burnley kwenye Ligi Kuu England Jumamosi iliyopita na kufanya Arsenal iwe imeshinda mechi zake zote mbili za kwanza msimu huu. Staa mwingine aliyefunga ni pacha wake, Lacazette, Pierre-Emerick Aubameyang. Tayari hadi sasa fowadi huyo wa Gabon, ameshafunga mabao mawili, akiwa alifunga pia kwenye mechi ya kwanza kabisa kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle United.
Pacha ya Aubameyang na Lacazette kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita ilikuwa moto, ambapo wa kwanza alifunga 22 na mwingine 13. Msimu huu, kocha Unai Emery anakwenda kuwatesa wapinzani wake na bunduki hizo, huku akiziongezea nguvu zaidi kwa kumleta kiungo mpishi, Dani Ceballos na winga matata, Nicolas Pepe. Kocha Emery ameboresha pia kwenye safu yake ya ulinzi, akimleta David Luiz kufunga duka kabisa.
Lacazette alisema: “Ligi Kuu England inaonekana kuwa nzuri sana kwa Lacazette, lakini ule ubora wa Lacazette bado haujaanza. Nataka kufunga mabao mengi zaidi, nataka kulinda kiwango changu kwa mechi zote.”
Mashabiki wa Arsenal sasa wamekuwa na uhakika. Kwa sababu wanachokiamini kwa sasa wamepata mrithi sasa wa Santi Cazorla baada ya kumnasa Ceballos. Kwenye mchezo wa Burnley, Ceballos, anayekipiga kwa mkopo Emirates akitokea Real Madrid, aliasisti mabao yote mawili na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.
Mechi ijayo, Arsenal watakipiga na Liverpool na kwamba kocha Emery amedaiwa huenda akaanza na bunduki zake tatu kwenye fowadi kwa maana ya Lacazette, Aubameyang na Pepe. Kwa msimu uliopita, Lacazette na Aubameyang walihusika kwenye mabao 51 na kwamba walizidiwa na pacha ya Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino waliohusika kwenye mabao 69 na kwamba hao walikuwa watatu, wao wawili tu. Sasa Pepe ameongezeka kwenye chama hilo la huko Emirates na kusisitwa kwamba moto wa kikosi hicho utakuwa mgumu kuzimwa.
“Tunakwenda Anfield tukiwa na pointi sita tulizobeba kwenye mechi mbili. Hiyo wiki itakuwa na mechi muhimu sana kwa kila shabiki wa Arsenal,” alisema Emery.