Mziba: Kuongoza Yanga si kufanya ubishoo ni vita kweli

Muktasari:

Wagombea watafanyiwa usaili kwa siku tatu kuanzia Jumapili, baada ya kupita katika mchujo wa awali uliofanyika hivi karibuni

Dar es Salaam.Wakati wagombea wa nafasi mbalimbali wakihesabu saa kabla ya kuingia kwenye hatua ya pili ya usaili utakaoanza Jumapili, mwanachama wa klabu hiyo na nyota wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’, amewaambia wagombea kuwa kuongoza klabu hiyo kunahitaji weledi wa hali ya juu.
Nyota huyo amekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba, hali iliyopo Yanga hadi kufikia kuchangishana kwa ajili ya timu kumetokana na uongozi kutetereka, hivyo watakaoingia wajifunze kutokana na makosa.
"Viongozi waliojitokeza wasichukulie nafasi hiyo kama kufanya 'show off' ili waonekane na kuongeza CV, la hasha, wawe na nia ya kujitolea na maono ya uongozi," alishauri Mziba.

Alisema wanawafahamu wote waliochukua fomu ni wanachama halali wa Yanga, lakini wakaiongoze Yanga kwa mapenzi na kujitolea na si kutaka wao waneemeke kupitia Yanga.

"Tunahitaji kutoka hapa tulipo, Yanga haikuwa timu ya kuchangishana, Yanga ni kubwa jamani, tuliyumba sababu uongozi haukuwapo na sababu zinajulikana, hivyo tusije kurudi tulikotoka," alisema.
Straika huyo wa zamani aliyesifika kwa kufunga magoli mengi ya kichwa, alisema viongozi watakaopewa ridhaa ya kuongoza klabu hiyo waangalie kwanza maslahi ya klabu na si matumbo yao.
"Tunahitaji mfumo mzuri, angalia wenzetu Simba, wanafanya vizuri na wanatamba kuwa wana kikosi kipana. Ni kweli, sababu tu wameona mbali, huko ndiko Yanga tunahitaji kwenda, ikiwezekana kuizidi hata Simba kwani Yanga ni kubwa kuliko timu yoyote nchini," alimaliza Mziba.
Yanga itafanya uchaguzi wake Mei 5 jijini Dar es Salaam kumpata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji waliojiuzulu kwa nyakati tofauti.
Wagombea watafanyiwa usaili kwa siku tatu kuanzia Jumapili, baada ya kupita katika mchujo wa awali uliofanyika hivi karibuni.
Awali uchaguzi huo ulipigwa danadana kutokana na mvutano uliokuwa ukiendelea kati ya baadhi ya wanachama, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali ambapo baadhi ya wanachama wa Yanga walikwenda kupinga mchakato mahakamani na uchaguzi ukasitishwa siku moja kabla ya siku iliyopangwa ufanyike.
Hata hivyo, wagombea waliokuwa wamejitokeza awali na wagombea wa sasa wote wamejumuishwa kwenye kinyang'anyiro hicho.