Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwenye Yanga yake karudi, Fei Toto nje mwezi

Golikipa wa Yanga Djigui Diarra.

SIKIA hii. Mshindani mkubwa wa Aishi Manula wa Simba ni Djigui Diarra wa Yanga anayerejea leo Jijini Dar es Salaam akitokea kwenye Afcon ambako timu yake ya Mali ilitolewa hatua ya 16 Bora. Tangu Diarra aende Afcon, Aishi amecheza mechi nne na kuambulia pointi nne kwenye Ligi Kuu Bara. Mashabiki wa Yanga wanamsubiri kwa hamu Diarra kujiunga na kambi yao inayoanza leo kujiandaa na mechi ya Ligi dhidi ya Mbeya City itakayopigwa Jumamosi pale kwa Mkapa.

Lakini Diarra anarejea katika kipindi ambacho langoni anamkuta kipa mpya, Aboutwalib Mshery, aliyesajiliwa katika dirisha dogo la uhamisho akitokea Mtibwa Sugar, akiwa gari limewaka ile mbaya.

Diarra anatarajiwa kuchukua namba yake kikosini hata kama haitakuwa dhidi ya Mbeya City, ambao waliizamisha Simba 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine Januari 17, lakini bado uamuzi mzito unabaki mikononi mwa kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi kuhusu nani aanze katika mechi hiyo ya Jumamosi.

Diarra hakupata nafasi ya kudaka katika Afcon ya nchini Cameroon iliyofikia hatua ya nusu fainali hivi sasa, lakini uzoefu wake unatarajiwa kumbakisha kuwa namba moja katika kikosi cha Nabi huku Mshery akitarajiwa kumpa ushindani wa uhakika.

Mbali na mechi tatu za Kombe la Mapinduzi Zanzibar ambako Yanga walitolewa kwa penalti katika nusu fainali dhidi ya Azam FC, Mshery amesimama langoni katika mechi nyingine tatu za Ligi Kuu Bara ambazo hajaruhusu bao hata moja dhidi ya Dodoma Jiji (4-0), Coastal Union (2-0) na Polisi Tanzania (1-0) na amedaka pia mechi nyingine moja ya Kombe la Shirikisho (ASFC) waliyoshinda 1-0 dhidi ya Mbao FC.

Kocha Nabi atakuwa na mtihani wa kuamua nani asimame langoni wakati wa mechi na Mbeya City kabla ya kuwavaa Biashara United katika mechi ya hatua ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Februari 12 hadi 17, mwaka huu.

Yanga imeanza mazoezi yake jana na leo wachezaji wanaingia rasmi kambini kujiandaa na mechi hizo lakini itawakosa baadhi ya nyota wao ambao ni majeruhi akiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayesumbuliwa na nyama za paja na atakuwa nje mwezi mmoja, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Yacouba Sogne na Kibwana Shomary ingawa hawa watatu wameanza mazoezi mepesi.

Katika mazoezi ya jana pia iliwakosa nyota Said Ntibazonkiza, Kocha Msaidizi Cedric Kaze ambao wapo kwao Burundi kwa ruhusa maalumu kama ilivyo kwa Heritier Makambo, huku Djuma Shabani na Yanick Bangala nao wakiwa kwenye timu yao ya taifa ya DR Congo iliyokuwa ikicheza mechi ya kirafiki.

Nabi alisema hivi sasa ratiba ya mazoezi inayofuata ni kurudisha miili ya wachezaji katika utimamu na hali ya kiushindani na ndani yake watafanya mazoezi ya mbinu kulingana na kile walichokionyesha katika mechi iliyopita na Mbao.

“Kuna maeneo tulifanya makosa hapo tutapambana kurekebisha ili kuondoa makosa hayo katika mechi zijazo na tulipokuwa imara kuboresha ili kufanya vizuri zaidi, akili yetu na nguvu sasa ni mechi ya Mbeya City tufanye vizuri kwa kupata ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kumalizana na Mbeya City na kufahamu tulichokipata akili na nguvu zitahamia michezo inayofuata ikiwamo ya Biashara na ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar tutakayokuwa ugenini.”


ASFC KAZI IPO

Yanga itakutana na Biashara United kwa mara ya tatu mfululizo kwenye mechi ya ASFC ambapo rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ndiyo imefanya vizuri zaidi ikitoka sare bao 2-2 na kufuzu kwa penalti 5-4, msimu uliopita Yanga pia ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Yacouba ambaye sasa ni majeruhi.

Kocha wa Biashara, Vivie Bahati alisema timu itakayojiandaa vyema ndiyo itakayoshinda.