Mwamnyeto: Tulieni, Yanga bado ina nafasi
Muktasari:
- Katika msimu wa kwanza wa kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, Yanga ilipangwa pia Kundi D na kumaliza mkiani ikikusanya pointi mbili zilizotokana na sare mbili, huku ikipoteza nne katika mechi sita ilizocheza, ikifunga pia mabao matano tu na kufungwa 19.
WAKATI mashabiki na wapenzi wa Yanga wakiingiwa ubaridi kutokana na timu hiyo kulazimishwa sare ya pili mfululizo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nahodha wa kikosi hicho, Bakar Mwamnyeto amewatuliza kwa kusema nafasi bado ipo kwani mechi mbili za uwanja wa nyumbani ndizo zitakazowavusha salama.
Yanga jana usiku ililazimishwa sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana katika mechi ya raundi ya tatu ya Kundi D na kufikisha pointi mbili ikiendelea kubaki mkiani na sasa imesaliwa na michezo mitatu, ikiwamo miwili ijayo ya nyumbani ukiwamo wa marudiano dhidi ya Medeama na ule wa Cr Belouizdad ya Algeria.
Hata hivyo, nahodha huyo wa Yanga, alisema baada ya bao la pili kukataliwa na mwamuzi katika mechi dhidi ya Medeama bado wachezaji walisalia katika morali kwani kutambua maamuzi ya refa hayapingwi na kushukuru kupata pointi moja na ugenini kwani anaamini wana nafasi ya kusonga mbele kutinga robio fainali ya ligi hiyo.
Mwamnyeto alisema mara baada ya mchezo huo wa Kumasi, Ghana Kocha Miguel Gamondi aliwapongeza kwa kuonyesha kiwango bora licha ya kutokupata matokeo na kuwaambia bado wana nafasi ya kushinda kwani kundi lipo wazi hadi sasa baada ya suluhu ya Al Ahly na CR Belouizdad kwenye pambano lililopigwa Cairo.
"Tunarejea nyumbani na tunarekebisha matokeo na mazoezini kufanyia kazi makosa yote tuliyoyafanya, kwani kocha atakuwa ameshajua nini cha kuboresha na tunashukuru kwa kututia moyo kwa kutuambia kundi liko wazi bado na ukweli ni kwamba tuna mechi mbili za nyumbani tumepania kushinda ili tujiweke pazuri kundini," alisema Mwamnyeto anayecheza kama beki wa kati wa timu hiyo na Taifa Stars.
"Hakuna kingine zaidi ya ushindi tu katika uwanja wa nyumbani ili kujiweka katika mikono salama kwani wanaocheza wote ni mabingwa wa nchi, hivyo kupata sare ugenini ni jambo la kawaida japo tutalifanyia kazi kuzidi kuwapa furaha mashabiki wetu wanaoendelea kutuunga mkono," aliongeza Mwamnyeto.
Yanga itarudiana na Medeana Desemba 20 kabla ya kuikaribisha Belouizdad mwishoni mwa Februari mwakani na kumalizana na Al Ahly mapema Machi baadae jijini Cairo na timu mbili zitakazoshika nafasi za juu za kundi zitafuzu robo fainali kuungana na timu nyingine sita za makundi mengine ya A, B na C.
Wababe hao wa Tanzania wanashiriki makundi kwa mara ya pili baada ya awali kutinga mwaka 1998 ikiwa ni miaka 25 iliyopita ilipoandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza nchini kufika hatua hiyo mara Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilipobadilisha mfumo kutoka Klabu Bingwa kuwa Ligi ya Mabingwa 1997.