Mwambusi: Yanga? Liwalo na liwe

HALI ikiwa bado tete kwa kikosi cha Ihefu, leo kitakuwa na wakati mgumu kuwakabili mabingwa watetezi Yanga katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, huku kocha mkuu wa timu hiyo ya Mbarali, Juma Mwambusi akisema ‘liwalo na liwe’.

Ihefu imekuwa na msimu mgumu katika ligi ikiwa imeshinda mechi mbili, sare mbili na kupoteza tisa katika mechi zake 13 za kwanza kufikia sasa na iko mkiani ikiwa na pointi nane, wakati Yanga iko kileleni kwa pointi 29.

Timu hizo zinakutana ikiwa ni mara ya tatu ikiwamo mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ambazo Yanga imeshinda zote na leo itakuwa ikisaka rekodi ya kwanza kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbarali, Mbeya itakakopigwa mechi hiyo.

Mwambusi alisema baada ya kupoteza mechi nyingi leo Jumanne wanaenda kupambana tena wakihitaji pointi tatu na kwamba watashambulia mwanzo mwisho kusaka mabao.

Alisema anaifahamu vyema Yanga, huku akieleza kuwa msimu huu wapinzani hao wamekuwa na mwenendo mzuri, hivyo watawaheshimu lakini si kuwaogopa bali dakika 90 ndizo zitaamua.

“Litakalokuwa na liwe, tutacheza mpira dakika 90 ndizo zitaamua, tunawaheshimu wapinzani kwakuwa wamekuwa na msimu mzuri ila tutapambana nao kadri ya uwezo wetu kusaka pointi tatu,” alisema.

Alisema katika mechi iliyopita dhidi ya Geita Gold waliyopoteza kwa bao 1-0, aliona upungufu haswa eneo la ushambuliaji, hivyo anaamini marekebisho atakayofanya yatabadili upepo.

Yanga iko katika ubora na itakuwa ikisaka kuboresha rekodi yake kufikia kucheza mechi 50 mfululizo za Ligi Kuu bila ya kupoteza.

Mdau wa soka jijini Mbeya, Hussein Dickson alisema: “Itakuwa ngumu sana kwa Ihefu kwasababu haijawahi kushinda dhidi ya Yanga.”