Mwamakula buana, eti hata Mayweather aje

MDAU gani wa ngumi asiyemjua Floyd Mayweather? Sio kwa mkwanja mrefu alionao ama umahiri wake ulingoni na zile mbwembwe zake za kimjinimjini!
Sasa msikie bondia Amos Mwamakula ambaye amefumba macho na kujidai eti hata mkali huyo wa masumbwi wa Marekani akija mbele yake, lazima achezee cha chembe.
Mwamakula aliyewahi kuishi Brazil kwa kipaji chake cha ngumi, aliamua kuwachekesha walionuna kwa kudai yeye ndiye mkali wao Bongo.
Yote tisa, bondia huyo alienda mbali na kudai eti akicheza hapa Bongo hawezi kupigwa hata apande ulingoni na Mayweather kwani lazima apigike tu.
Sasa haijulikani alikuwa akimtaja Money Man ambaye siku chache zijazo atazichapa na Conor McGregor au kuna Mayweather Chips wa pale Kinondoni?!
“Mimi sio bondia wa kupigwa nyumbani, hata aje Mayweather, lazima apigike, nimeoga maji ya Ziwa Nyasa, sipigiki kizembe kabisa,” alitamba Mwamakula wakati akizungumzia pambano lake na Willson Matamba wa Malawi la kuwania ubingwa wa UBO Afrika la uzani wa Light.
Pambano hilo litafanyika Agosti 12 kwenye Ukumbi wa Travertine, Dar es Salaam likitanguliwa na pambano la Japhet Kaseba atakayezichapa na Seleman Said ‘Tall’ kuwania ubingwa wa Taifa kwenye uzani wa super middle.
Mratibu wa pambano hilo, Kwame Nkuruma alisema kuwa siku hiyo itapigwa michezo minane mikubwa likiwamo la Ibrahim Tamba dhidi ya Imani Mapambano, Hamza Mchanjo dhidi ya Ally Jangalaga, Shaaban Kaoneka atakayecheza na Kanda Kabongo.