Mwakinyo amfanyizia Mkongo

Muktasari:
Ushindi huo umemfanya bondia huyo kuwamwagiwa sifa Watanzania kwa kumpa sapoti hata kabla ya kupanda ulingoni na kudai huo ni mwanzo tu kwani safari ya kuweka rekodi kwenye ngumi za kimataifa inaendelea
BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ameendeleza makali yake baada ya kumfanyizia Mkongoman, Tshibangu Kayembe kwa kumshinda kwa pointi kwenye pambano lao la kuwania mkanda wa Mabara wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (WBF)
Mwakinyo alishinda pambano hilo la uzani wa SuperWelter la rundi 12 kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililochezwa usiku wa kuamkia leo lililosindikizwa na mapambano kadhaa ya utangulizi yakiwamo ya mabondia wa kike.
Ushindi huo umemfanya bondia huyo kuwamwagiwa sifa Watanzania kwa kumpa sapoti hata kabla ya kupanda ulingoni na kudai huo ni mwanzo tu kwani safari ya kuweka rekodi kwenye ngumi za kimataifa inaendelea.
Katika pambano hilo lililochezwa na mwamuzi Upendo Njau, Mwakinyo alipewa ushindi na majaji wote watatu kwa pointi 116-112, 119-109 na 119-109.
Mara baada ya pambano hilo, Mwakinyo aliandika kwenyue ukurasa wake wa twitter akisema;
SALA,NIDHAMU,JUHUDI NA UVUMILIVU = MAFANIKIO
"Ushindi Wangu Wa Leo ni Maalumu kwa Taifa Langu, Natamani Ushindi Huu Ukawe Mfano Kwa Mabondia Wengine Nawashukuru Sana Watanzania Kwa Sala, Dua Na Sapoti zenu Katika Kufanikisha Hili."
Katika mapambano ya utangulizi mambo yalikuwa hivi;
Juma Habib alipigwa kwa pointi na Abdul Juma, Hamidu Kwata alimpiga kwa KO ya raundi ya kwanza katika dakika mbili na sekunde 15 Ayubu Ula naye Mussa Nassor alimchapa kwa pointi Ajemi Aman katika pambano la raundi sita la Super Walter.
Kwenye pigano la wanawake la uzito wa Light, Feriche Mashauri aka Boyka alimchapa Hajjath Shomari 'Mawe kama Relini kwa pointi, huku Issa KIbwana naye akitakata kwa pointi dhidi ya Abdallah Lioba na kwenye uzito wa Fly, Stumai Muki alimpiga kwa pointi Leila Yazidu.
Kwenye uzito wa Super Feather, Issa Nampepeche alimdunda kwa KO, Khalid Manje katika pambano lao. Manje alipigwa katika raundi ya pili ya pambano hilo, huku Ismail Gariatano 'Mwanajeshi' alishinda kwa pointi dhidi ya Said Zungu katika uzani wa Super Bantam.
Bondia mwingine Emmanuel Mwakyembe alipigwa kwa pointi katika uzito wa Super Feather la raundi nane dhidi ya Juma Choki, huku Haidari Mchanjo na Baina Mazola walitoshana nguvu kwa kutoka sare kwenye pambano la uzani Feather.
Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya ngumi, Seleman Kidunda naye alimtwanga Shaaban Kaoneka na kumstaafisha ngumi baada ya kumpiga kwa TKO ya raundi ya kwanza tu baada ya mpinzani wake huyo kuumia bega kabla ya kutangaza kuachana na ngumi.
Katika pambano hilo la uzani wa Super Middle la raundi nane, Kaoneka alionekana akiwapungia mkono mashabiki kisha kutangaza anaachana na ngumi kwani alihisi angekufa uwanjani kwa vile alipamba akiwa ana malaria, ila alishaingia mkataba akaona lazima apigane kutimiza wajibu.
Kabla ya Mwakinyo hajaonyeshana kazi na Kayembe, Tony Rashid alifungua njia kwa Watanzania baada ya kumtwanga Mmalawi, Yamikani Mkandawire katika pambano la raundi 10 la uzani wa Super Bantam kwa kumtwanga mpinzani wake kwa KO ya raundi ya pili.