Mvua yasimamisha mazoezi Yanga

Mvua kubwa inayonyesha mkoani Mtwara jioni ya leo Mei 16  imesimamisha kwa muda mazoezi ya Yanga yanayofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.
Yanga ambayo jana ilitoka suluhu na Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa, Ruangwa baada ya mchezo huo iliondoka usiku huo huo na kuja kuendelea na kambi yao mkoani Mtwara waliyoweka tangu Jumatano iliyopita.
Leo ratiba ya mazoezi ya timu hiyo iliendelea na ilikuwa ianze saa 10:00  Jioni licha ya timu hiyo kutinga kwenye uwanja wa Nangwanda majira ya saa 10:10 .
Baada ya basi la timu hiyo kufika wachezaji wote walishuka nakuingia uwanjani isipokuwa Deus Kaseke na kipa Ramadhan Kabwili ambayo walikaa pembeni kwani walikuwa wakijisikia vibaya.
Hata hivyo dakika 10 tu tangu timu hiyo ianze mazoezi mepesi ya kupasha misuli mvua kubwa ilianza kunyesha ndipo kocha Nasreddine Nabi aliwaita wachezaji wote na kuwataka kuingia kwenye basi.
Licha ya kuwataka wote kuingia kwenye gari hata hivyo hakutoa koni na vifaa  vya mazoezi ambavyo Bado viko ndani ya uwanja hali inayoonyesha kuwa wanasubiri kama mvua itaisha wanaweza kuendelea na mazoezi.
Bado wachezaji na makocha wameendelea kukaa kwenye basi huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha na kama hali iliendelea hivi kwa muda mrefu kocha Nabi anaweza kuvunja mazoezi na timu  kurejea kambini.