Musonda, Doumbia wafumua mifumo Yanga

MASHABIKI wa Yanga walikuwa wanalia na kocha wao Nasreddine Nabi juu ya mifumo yake na sasa yule straika Mzambia ameshamaliza utata na jamaa anaanza nao, huku beki wa kati Mamadou Doumbia naye akija kuufumua ukuta wa timu hiyo ikielezwa itaibeba ikicheza CAF.

Mtoto wa kocha wa Yanga, Hedi Nabi ambaye ni mtoto pekee wa kiume wa Nabi ameliambia Mwanaspoti kwa simu akiwa kwao Ubelgiji kuwa ujio wa Musonda sasa unakwenda kumrudisha baba yake katika mfumo mpya ambao uliwahi kumpa mafanikio makubwa Afrika.

Hedi alisema ujio wa Musonda sasa rasmi baba yake atarudi kutumia mfumo wa 4-4-2 ambao aliwahi kuujaribu mara moja tu akiwa Yanga kisha akaona hautaweza kumpa mafanikio anayoyataka.

Akifafanua zaidi akisema mfumo huo wa 4-4-2 utarejea Yanga kutokana na ujio wa Musonda ambaye ubora wake utampa nafasi baba yake kumtanguliza mbele kucheza sambamba na kinara wa mabao kwa timu hiyo na ligi Fiston Mayele.

“Unajua baba aliwahi kujaribu huu mfumo wa 4-4-2 wakati Makambo (Heritier) alipokuwa hapo mara moja, lakini hakuona kama umefanikiwa, alifanya hivyo ili acheze pamoja na Fiston (Mayele),” alisema Hedi anayesomea taaluma ya kuchambua mechi.

“Nimemuona Musonda (Kennedy) kwa ubora alionao nadhani sasa baba atarudi katika mfumo wa 4-4-2 ili acheze sambamba na Fiston nadhani hapo kutakuwa na timu bora zaidi, ambayo nilikuwa naona muda mrefu mashabiki walikuwa wanataka hilo mitandaoni.”

Tangu atue Yanga Nabi alikuwa akitumia hasa mfumo wa 4-2-3-1 ambao ulimfanya kutumia mshambuliaji mmoja pekee mbele huku wengi wakiwa viungo ambapo hata alipobadilisha alitumia mfumo wa 4-3-3.

Aidha, Hedi alikiri ujio wa mfumo huo unaweza kuwa sio habari njema kwa viungo wengi wa timu hiyo kutokana na idadi yao ambapo utalazimika kutumia mawinga wawili na viungo wawili pekee.

“Nafikiri changamoto kubwa kwa baba na hata viungo wa Yanga ni ubora wa viungo waliopo, kwasababu timu ikitumia mfumo huo italazimisha idadi kidogo ya viungo kutumika katika mfumo mmoja.

“Upande mwingine itakuwa ni faida kwa timu kwani pia kocha anaweza kubadili na kurudi kwenye mfumo wa 4-2-3-1 kama akiona inahitajika,” alisema,

“Kila mchezaji anauchezaji wake nafurahia ujio wake naamini utaongeza chachu ya ushindani kikosini lakini sina hofu yoyote nitapambana kuhakikisha naendelea kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kama ilivyo sasa.”