Mukwala, Ahou waanza kutupia Simba

Muktasari:
- Mukwala alikuwa katika presha kubwa kufuatia kushindwa kuonyesha makali yake katika michezo minne iliyopita, mmoja wa kilele cha Simba Day dhidi ya APR ya Rwanda, miwili ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union na mmoja wa ligi dhidi ya Tabora United.
Licha kupoteza nafasi tatu za wazi ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, mshambuliaji wa Simba raia wa Uganda, Steven Mukwala ameanza kucheka na nyavu baada ya Simba kushinda mabao 4-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa KMC Complex.
Mukwala alikuwa katika presha kubwa kufuatia kushindwa kuonyesha makali yake katika michezo minne iliyopita, mmoja wa kilele cha Simba Day dhidi ya APR ya Rwanda, miwili ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union na mmoja wa ligi dhidi ya Tabora United.
Mbali na Mukwala mchezaji mwingine aliyeonyesha makali kwenye mechi hii ni Jean Charles Ahoua ambaye alifanikiwa kufunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.
Simba ilianza kufunga bao kupitia kwa Edwin Balua katika dakika ya 13 ambaye alipata pasi safi toka kwa Ahoua, hili likiwa ni bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Dakika ya 44, Mukwala alifunga bao safi akipata pasi nzuri kutoka kwa beki Shomary Kapombe, likiwa ni bao ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki.
Kipindi cha pili bado hakikuwa kizuri kwa Fountain ambao waliendelea kufanya makosa mengi kwenye eneo la ulinzi na kumruhusu Ahoua afunge bao lake la kwanza kwenye ligi katika dakika ya 59 akipokea pasi ya Muhammed Hussein ‘Tshabalala’.
Ahoua aliendelea kuonyesha makali yake tena kwenye mchezo huu baada ya kumpa pasi safi Valentino Mashaka ambaye alifunga bao lake la pili kwenye Ligi Kuu msimu huu na kuipa Simba ushindi huo muhimuambao umeirudisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita na mabao saba, lakini ikiwa haijaruhusu bao lolote katika mechi mbili.
“Bado tuna kazi ya kufanya, nafikiri tutarudi mazoezini ili kuendelea kutafuta makali zaidi kwenye michezo ijayo,” alisema kocha wa Simba, Fadlu Davids.