Mugalu Yanga freshi, Lwanga bado

KATIKA mechi ya dabi leo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba, watamkosa kiungo wao mkabaji, Taddeo Lwanga kutokana na majeraha ya goti ambayo bado yanamsumbua.
Ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzale amesema Lwanga hata kambini hayupo kutokana na majeraha yake hayo yupo nchini ya kikosi maalumu kwa ajili ya matibabu.
Barbara amesema Lwanga anaendelea vizuri na matibabu yake ili apone kabisa na kurudi kujiunga na wachezaji wenzake katika majukumu ya timu ila leo hatakuwepo.
Amesema Lwanga akirejea kabla ya kuanza mazoezi na wenzake jopo la madaktari wa Simba watamuangalia na kumfanyia tathimini ya kutosha ili kuona kama matatizo yake yameisha.
"Kuhusu straika wetu Chriss Mugalu yupo sehemu ya kikosi kilichokuwa kambini na alifanya mazoezi ya pamoja kama wachezaji wengine walivyokuwa wakitimiza majukumu yao," amesema Barbara na kuongeza;
"Katika mazoezi kwa nafasi yangu Mugalu alifanya vizuri ila jukumu la kucheza mechi ya leo dhidi ya Yanga au kuwekwa benchi si jukumu langu bali ni la kocha wetu, Pablo Franco,"
"Ambacho nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao kwani Mugalu na wachezaji wengine wote waliokuwa kambini wana hali na morali kubwa ya kuipigania Simba na kuona tunashinda."