Mtihani wa Chole MVP wa AFCON U17
Muktasari:
- Katika fainali hizo zilizofanyika Morocco, licha ya timu hiyo kukosa ubingwa huo, ila ilishuhudiwa kiungo wa Serengeti Boys, Issah Chole akitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano yaani (MVP), baada ya kuonyesha kiwango cha kuvutia zaidi.
MICHUANO ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U17), imefikia tamati Juni 2, 2026, huku ikishuhudiwa Serengeti Boys ikikosa ubingwa baada ya kufungwa na Senegal kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wa fainali.
Katika fainali hizo zilizofanyika Morocco, licha ya timu hiyo kukosa ubingwa huo, ila ilishuhudiwa kiungo wa Serengeti Boys, Issah Chole akitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano yaani (MVP), baada ya kuonyesha kiwango cha kuvutia zaidi.
Hata hivyo, licha ya Issah Chole kutwaa tuzo hiyo, ila anakabiliwa na kibarua cha kufuata nyota ya mastaa wengine kibao waliotamba katika mashindano hayo, ambao wanacheza Barani Ulaya, huku yeye akiwa anaitumikia Klabu ya Fountain Gate FC.
Katika fainali za michuano hiyo ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17, zilizofanyika Gabon mwaka 2017 na Mali kuchukua ubingwa, mchezaji bora alikuwa ni Zito Luvumbo wa Angola ambaye kwa sasa anaichezea Klabu ya RCD Mallorca ya Hispania.
Luvumbo alianza karia yake ya soka katika Klabu ya Primeiro de Agosto ya kwao Angola, kisha baadaye kwenda kufanya pia majaribio kwenye akademia ya Manchester United ya England, Februari 2019, kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho.
Fainali za mwaka 2019, zilizofanyika Tanzania mchezaji bora alikuwa ni Steve Mvoue aliyeiwezesha Cameroon kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, ambapo kwa sasa kiungo huyo nyota anaendelea kuonyesha kipaji chake na Klabu ya IK Start ya Norway.
Katika fainali za mwaka 2023, zilizofanyika Algeria na bingwa kuibuka Senegal, mchezaji bora wa michuano hiyo alikuwa ni Souleymane Alio wa Burkina Faso, ambaye kwa sasa anaendelea kufanya vizuri na kikosi cha FC Nordsjælland ya Denmark.
Fainali za mwaka 2025, zilizofanyika Morocco na wenyeji kutwaa ubingwa huo, nyota wa timu hiyo, Abdellah Ouazane ndiye aliyetwaa tuzo mchezaji bora, akifunga mabao mawili na kutoa asisti tatu, ambapo kwa sasa anaichezea AFC Ajax ya Uholanzi.
Kwa maana hiyo, wachezaji wote bora waliotokea katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U17), tayari wanaendelea kuonyesha vipaji vyao Barani Ulaya, jambo ambalo ni deni kwa Chole kuendelea kung’ara zaidi.
Hata hivyo kinda huyo ndiye mchezaji pekee ambaye timu yake haijatwaa ubingwa huo lakini amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo muhimu kwenye mashindano.
Akizungumza na Mwanaspoti Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau amesema yapo mazungumzo na timu mbalimbali kutokea Bara la Ulaya ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji mchezaji huyo kwa ajili ya majaribio, ingawa bado ni mapema kuzungumzia hilo.
“Wachezaji wetu wawili kwa maana ya Juma Issa Abushiri ‘Messi wa Chuga’ na Issah Chole tayari kuna mazungumzo na timu za nje zinazowahitaji, ila suala lao kuna watu muhimu ambao tumewaachia waendelee kulishughulikia kwanza,” amesema Makau.
Mwanaspoti linatambua, Juma Issa Abushiri ‘Messi wa Chuga’ anayecheza timu ya wakubwa ya Fountain Gate na Issah Chole anayecheza kwa vijana, wanawindwa na Klabu za Olympique Marseille ya Ufaransa na SK Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech.