Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Machozi ya Serengeti Boys yanavyofungua fumbo la kesho

ZENGWE Pict


FAINALI za Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) mwaka 2026 zilizofanyika nchini Morocco zimetoa sababu kubwa ya Watanzania kujivunia kizazi kipya cha soka.


Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la vijana Afrika Mashariki, Serengeti Boys imefika hatua ya fainali na kushiriki mchezo wa mwisho wa mashindano hayo, kabla ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Senegal.


Matokeo ya mwisho yanaweza kuonyesha Tanzania imepoteza ubingwa, lakini kwa wengi waliofuatilia mchezo huo kwa ukaribu, habari kubwa si kupoteza kwa penalti bali ni namna timu ilivyoweza kushindana kwa kiwango cha juu dhidi ya wapinzani wao.

SERE 02

Serengeti Boys walionyesha uwezo mkubwa wa kiufundi na kimbinu, jambo ambalo limekuwa nadra kuonekana kwa timu nyingi za taifa katika ngazi za vijana.

Katika mchezo huo, vijana wa Tanzania walifanikiwa kutafsiri vizuri nyakati tano muhimu za mchezo wa soka. Walikuwa na uwezo mzuri walipokuwa wanamiliki mpira, walikuwa na nidhamu walipokuwa bila mpira, walionyesha uwezo wa kurejesha umiliki mara baada ya kuupoteza na pia walikuwa na mpangilio mzuri katika mipira ya kutenga. Haya ni mambo yanayoonyesha uwepo wa maandalizi bora na falsafa ya mchezo iliyofundishwa kwa umakini.

SERE 03

Mbali na mbinu za timu, wachezaji binafsi walionyesha kiwango kizuri cha ufundi na ujanja wa kisoka. Utambuzi wa mazingira ya mchezo, uamuzi sahihi pamoja na utekelezaji wa uamuzi huo vilikuwa sehemu ya nguvu kubwa ya Serengeti Boys katika michuano yote. Haya ndiyo mambo yanayowafanya Watanzania wengi kuamini kuwa kundi hili linaweza kuwa msingi wa mafanikio makubwa ya taifa katika miaka ijayo.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, ni muhimu kutambua kuwa hawa bado ni vijana wanaojifunza. Wanahitaji kuendelea kupewa nafasi ya kukua, kujifunza na kuendelezwa badala ya kubebeshwa mzigo mkubwa wa kulikomboa taifa mapema. Historia ya soka imeonyesha vipaji vingi vikiharibika kutokana na matarajio makubwa yasiyoendana na umri wao.

SERENGETI Pict

Wakati kila mmoja ana haki ya kushauri au kutoa maoni yake kuhusu maendeleo ya timu, tunapaswa pia kukumbuka kuwa wengi wa vijana hawa wanatoka katika klabu ambazo zina malengo na mipango yake ya maendeleo. Klabu zinahitaji kuendelea kushirikiana na timu za taifa ili kuhakikisha vipaji hivi vinakua katika mazingira sahihi bila kuathiri maendeleo yao ya muda mrefu.

Mafanikio haya pia yanapaswa kutufanya tuangalie kwa karibu kazi inayofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya uongozi wa Rais Wallace Karia pamoja na Idara ya Ufundi ya TFF. Licha ya changamoto mbalimbali za kifedha na miundombinu, wameweza kutengeneza kundi la vijana ambalo leo limeifanya Tanzania kutajwa miongoni mwa mataifa bora ya vijana barani Afrika.

SERE 02

Badala ya kujificha nyuma ya mafanikio haya na kuyatumia kama sehemu ya majigambo, wadau wote wa soka wanapaswa kujiuliza ni nini kinachofuata. Tunahitaji kuona mipango mikubwa zaidi ya kuwekeza katika vituo vya maendeleo ya vijana, viwanja vya mazoezi, programu za makocha pamoja na mashindano ya vijana yatakayowezesha kuzalishwa kwa vipaji vingi.

Hakika tunapaswa kuwapongeza vijana hawa kwa mafanikio yao. Lakini pongezi hizo ziambatane na mikakati ya muda mrefu ya kutengeneza kina Issa Chole, Athanas Dismas na vipaji vingine vingi zaidi. Pia tunahitaji kanuni na sera zitakazolinda maendeleo ya wachezaji wazawa wenye uwezo wa kushindana kwa ubora, si kwa sababu ya uzawa wao pekee.

SERE 01

Matarajio yangu ni kwamba wakati mwingine nitakapomsikia kiongozi wa serikali akizungumzia mafanikio haya, sitasikia tu pongezi kwa vijana hawa, bali pia nitasikia mpango wa kujenga miundombinu mipya, kuboresha miradi ya maendeleo ya vijana na kuweka mazingira yatakayowezesha maelfu ya watoto wa Kitanzania kuandaliwa kwa mahitaji ya soka la kisasa. Hapo ndipo tutakapokuwa tumelitendea haki somo kubwa ambalo Serengeti Boys wametuachia.