Mtibwa yahamishia hasira kwa KMC

Muktasari:
- Mtibwa Sugar juzi ilikumbana na kibano cha mabao 2-0 dhidi ya Singida BS ikiwa ni mchezo wa raundi ya 24 uliopigwa Uwanja wa Liti na kuendelea kubaki nafasi ya sita kwa pointi 29, huku wapinzani wakiwa nafasi ya nne kwa alama 47.
BAADA ya kuchezea kipigo juzi kwenye Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar imesema inaenda kusahihisha makosa yake na kumalizia hasira kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya KMC.
Mtibwa Sugar juzi ilikumbana na kibano cha mabao 2-0 dhidi ya Singida BS ikiwa ni mchezo wa raundi ya 24 uliopigwa Uwanja wa Liti na kuendelea kubaki nafasi ya sita kwa pointi 29, huku wapinzani wakiwa nafasi ya nne kwa alama 47.
Wakata Miwa hao wanatarajia kuwa nyumbani Uwanja wa Turiani mkoani Morogoro kuwakaribisha KMC Jumamosi katika hesabu ya kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
KMC itakuwa na kibarua kingine kigumu kwani haijapata ushindi kwenye mechi saba mfululizo za ligi kuu tangu ilipofanya hivyo Desemba 22, ilipoichapa Polisi Tanzania mabao 2-0.
Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma alisema kupoteza mechi ya juzi ilikuwa ni makosa ya timu nzima, hivyo wanaenda kujisahihisha kuhakikisha wanamalizia hasira zao kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya KMC.
Alisema wanafahamu mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wao kuhitaji ushindi ili kufuzu hatua inayofuata hivyo watakuwa makini sana ili kufikia malengo ya timu hiyo kusonga mbele.
“Kimsingi ni kusahau yaliyopita na kujipanga upya, tulifanya makosa ya kitimu, lakini hatukati tamaa tunaenda kujisahihisha na kurejesha morali upya kupitia mechi ijayo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya KMC,” alisema Juma.