Mtanzania ashiriki kuchagua wanamichezo ufadhili wa Sh4.6 Bilioni Anoca Paris 2024

Katibu Mkuu wa kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alikuwa miongoni mwa wajumbe saba wa kikao cha kamisheni ya kuchagua wanamichezo watakaofaidika na udhadhili wa Anoca Paris 2024 (Anoca Athlete Support Programme Paris 2024).

Kikao hicho cha siku mbili kilifanyika mjini Abuja Nigeria yalipo makao makuu ya Shirikisho la Kamati za Olimpiki za Afrika (Anoca) ikiwa ni muendelezo wa ufadhili wa mazoezi kwa wanamichezo wa Afrika, baada ya karibuni kitengo cha misaada (Olympic Solidarity) cha kamati ya Olimpiki ya kimataifa (IOC) kutoa ufadhili huo 'OS Athletes Scholarships Paris 2024' kwa wanamichezo watano nchini.

Wanamichezo hao waliotangazwa na TOC ni wanariadha, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Failuna Abdi, judoka, Andrew Mlugu na muogeleaji, Hilal Hilal ambao watalipwa dola 1500 kwa mwezi kila mmoja kuanzia Julai 2022 hadi Agosti 2024 kwa ajili ya maandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa 2024 ambao ni mpango wa dunia unaofaidisha Kamati za Olimpiki 206.

Mbali na IOC, Anoca pia imejitosa kuwafadhili wanamichezo wake ili wawe na uwezo kushinda medali kwenye Olimpiki ambayo msimu huu ufadhili wake ni mara mbili ya ule walioutoa kwenye maandalizi ya Olimpiki 2020.

"Kabla ya Olimpiki ya 2020 Anoca ilitoa ufadhili wa US$ 1.0 milioni (zaidi ya Sh 2.3 bilioni kwa vyama na mashiriki saba, msimu huu kwenye maandalizi ya Paris 2024, Anoca imewekeza US$ 2.0milioni (zaidi ya sh 4.6 bilioni) katika michezo ya riadha, ngumi, judo, kuogelea, mieleka, kunyanyua vitu vizito na taekwondo," amesema Bayi baada ya mkutano huo.

Amesema vigezo vya Anoca vimekuwa juu zaidi kulinganisha na vile vya Olympic Solidarity ambavyo vimewapa fursa nyota watano nchini kufaidika na ufadhili huo wa mazoezi akifafanua kwamba lengo na madhumuni ya Afrika ni kuona wanamichezo wa bara hilo watakaopewa ufadhili  wanakuwa kwenye jukwaa la medali (Medal Pordium) kwenye Olimpiki ijayo.

"Miongoni mwa vigezo vya ufadhili wa Anoca ni lazima anayepewa ufadhili huo awe ana medali yoyote katika Olimpiki ya  Tokyo 2020, awe katika nafasi 10 bora duniani katika michezo tajwa hapo juu, hadi Desemba 31, 2021 awe aliingia kwenye nafasi 10 bora katika michezo iliyo kwenye ratiba ya Paris 2024 na asiwe kati ya wachezaji waliopata ufadhili wa Olimpiki Solidariti.

"Kutokana na vigezo hivyo nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania haiwakuweza kuomba huku Kenya, Uganda, Algeria, Ethiopia, Cote’ Ivoire, Burkina Faso, Madagascar, Malawi, Botswana, Misri, Tunisia, Nigeria, Namibia, Afrika Kusini na Morocco ndizo zimefanikiwa kupata kati ya nchi 54 za Afrika zilizoomba ufadhili huo kwa kuwasilisha majina ya wanamichezo 102, wanawake 48 na wanaume 54.

Alifafanua kwamba, baada ya Kamisheni ya “ANOCA Athlete Support Paris 2024” iliyoongozwa na wajumbe sita akiwamo mwenyekiti Seydina Omar (Senegal), Ezera Tsebangu (mkurugenzi wa ufundi Anoca), Hashim Ahmed (katibu mkuu Anoca), Gumel Habu (mweka hazina wa heshima Anoca), Bayi, Tegla Leroupe (Kenya) na Faissal Raguib (Djibouti) ambao ni wajumbe, kukupitia majina hayo, 49 pekee ndiyo walikidhi vigezo vyote tajwa ambao ni wanawake 23 na wanaume 26 watakaonufaika na ufadhili huo.