Msuva, Sure Boy kukiwasha Morogoro

MASTAA kibao wanaokipiga Ligi Kuu Bara wanatarajia kuungana na mabeki wa Yanga, Dickson Job na Kibwana Shomari katika mchezo wa hisani wenye lengo la kuchangisha fedha kutoka kwa mashabiki na kusaidia jamii mkoani hapa.

Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Sabasaba kesho Julai 8 mwaka huu kuanzia saa 10 jioni huku Simon Msuva, Bakari Mwamnyeto, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, Salum Kihimbwa na wengineo watakuwapo.

Meneja wa wachezaji hao George Job alisema, kila mmoja ameunda kikosi kabambe cha mastaa wanaocheza ligi ili kushiriki mchezo wa hisani wenye lengo la kukusanya fedha na kusaidia watoto yatima na wanawake wajawazito.

Alisema fedha za kiingilio zitakazopatikana zitatumika kununua mahitaji yaliyobainishwa na uongozi wa walengwa.

“Mchezo huu umekuja na kauli mbiu ya ‘Wape Tabasamu’ ambapo Kibwana na Job wamekubaliana kila mmoja wao kuunda kikosi cha wachezaji ambao watawasapoti katika Team Kibwana na Team Job na fedha zitakazopatikana zitanunulia mahitaji kwa ajili ya kutoa msaada kwa watoto yatima na akinamama wajawazito.” alisema George.

Kibwana aliwataja baadhi ya wachezaji watakaokuwepo kumsapoti kuwa ni Msuva, kipa wa Dodoma Jiji, Dotto Masalanga, Nickson Kibabage (Mtibwa Sugar), Mwamnyeto, Lusanjo Mwaikenda (Azamu), Sure Boy (Yanga), Jafari Kibaya na Kihimbwa (wote Mtibwa Sugar) na wengine wengi.

Wakati kwa Job aliwataja baadhi ya nyota wake kuwa ni Shiza Kichuya (Namungo), Iddy Kipagwile (KMC Fc), Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ (Mtibwa Sugar), Haruna Chanongo (Ruvu Shooting), Aboutwalib Mshely (Yanga) na Hamad Waziri (Mbeya City).