Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msuva azungumza ishu ya kustaafu soka

Muktasari:

  • Msuva ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Al-Talaba SC ya Iraq, amesema anajiona bado yupo katika hali nzuri kimwili na kiushindani, jambo linalompa matumaini ya kuendelea kucheza katika kiwango cha juu kama ambavyo ameendelea kufanya nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo.

WAKATI wengi wakianza kuhesabu siku za mwisho za mastaa waliovuka miaka 30, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, ameeleza kwamba hana mpango wa kustaafu leo wala kesho na anaamini bado ana uwezo wa kucheza soka la ushindani kwa miaka kadhaa ijayo.

Msuva ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Al-Talaba SC ya Iraq, amesema anajiona bado yupo katika hali nzuri kimwili na kiushindani, jambo linalompa matumaini ya kuendelea kucheza katika kiwango cha juu kama ambavyo ameendelea kufanya nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Msuva mwenye miaka 32  alisema mfano wa Ronaldo umekuwa ukionyesha kuwa umri si kikwazo kwa mchezaji anayejitunza vizuri na kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika maisha ya soka.

"Watu wengi wanauliza nitastaafu lini lakini ukweli ni kwamba sina mpango wa kustaafu leo wala kesho. Nikiwa na afya njema na uwezo wa kushindana nitaendelea kucheza. Angalia Ronaldo bado anacheza katika kiwango kikubwa, inaonyesha kila kitu kinawezekana ukiwa na nidhamu," alisema Msuva.

Katika kusimamia hilo katika mapumziko yake ya mwisho wa msimu, Msuva ameendelea kufanya mazoezi binafsi katika fukwe za Coco jijini Dar es Salaam na gym mbalimbali akiamini mwili wa mwanasoka ni mtaji unaopaswa kutunzwa kila siku.

Kwa zaidi ya miaka tisa sasa, nyota huyo amekuwa akicheza nje ya Tanzania baada ya kuondoka Yanga kwenda Morocco kabla ya kuhamia Saudi Arabia na baadaye Iraq. Katika safari hiyo amejijengea heshima kubwa kama mmoja wa wachezaji waliofanikiwa zaidi kutoka Tanzania katika kipindi cha hivi karibuni.

Takwimu zake pia zinaonyesha bado ana mchango mkubwa uwanjani. Katika msimu wa 2024/25 akiwa na Al-Talaba alifunga mabao 13 na kutoa asisti sita, huku msimu uliomalizika hivi karibuni akifunga mabao tisa na kutoa asisti nne licha ya kukosa mechi kadhaa kutokana na majukumu ya timu ya taifa.

Ndani ya Taifa Stars, Msuva ameendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa zaidi. Ameshiriki kampeni mbalimbali za kufuzu AFCON na amebaki kuwa mmoja wa nyota waliotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya Tanzania kurudi kwenye michuano hiyo ya Afrika baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

Mbali na mafanikio yake binafsi, mshambuliaji huyo alisema anatamani kuona kizazi kipya cha wachezaji wa Tanzania kikifuata nyayo zake kwa kuthubutu kucheza nje ya nchi na kupambana katika ligi mbalimbali duniani.

Wakati akiwa Yanga, Msuva aliwahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili, akifunga mabao 17 msimu wa 2014/15 na mabao 14 msimu wa 2016/17, takwimu ambazo zilimfungulia mlango wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.