Nyota KMC wataka heshima
Muktasari:
- KMC imebakiza mechi dhidi ya Namungo FC, Mashujaa na Simba hivyo ikitokea imeshinda itafikisha jumla ya pointi 18, hilo linathibitisha timu hiyo kushuka daraja moja kwa moja.
INGAWA katika mechi tatu zilizobakiza kwa KMC, ikitokea ikashinda zote hazitabadilisha chochote kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, pamoja na hilo nyota wa timu hiyo, wamesema haimaanishi wamekata tamaa kupambana na kuonyesha uwezo wao.
KMC imebakiza mechi dhidi ya Namungo FC, Mashujaa na Simba hivyo ikitokea imeshinda itafikisha jumla ya pointi 18, hilo linathibitisha timu hiyo kushuka daraja moja kwa moja.
Miongoni mwa nyota wa KMC waliyozungumza na Mwanaspoti ni mshambuliaji Darueshi Saliboko aliye na mabao matano alisema jukumu lao ni kuendelea na mapambano hadi mechi ya mwisho bila kujali timu imeshuka.
"Haijalishi timu imeshuka, lazima tuendelee kupambana na tunafanya mazoezi kwa kujituma, naamini tunachokionyesha uwanjani pia kinaonekana, mchezaji huwezi kusema kwa kuwa timu haikuwa na matokeo ya kushinda kwa hiyo ujibweteke," alisema Saliboko na kuongeza;
"Mfano Kagera Sugar msimu uliyopita licha ya kushuka ilipambana hadi hatua ya mwisho, haikukata tamaa ikapambana Ligi ya Championship imepanda tena, mpira wa miguu una matokeo ya kufurahisha na kuumiza, unapoumia siyo mwisho wa safari."
Kwa upande wa kiungo mshambuliaji, Rashid Chambo aliye na mabao matatu alisema:"Tutaendelea kupambana hadi dakika 90 za mwisho, kwani licha ya timu kushuka lazima kuipa thamani timu, tunajitahidi kuwa na utulivu na kujituma kwa bidii."
Mwingine aliyechangia hilo ni kiungo wa timu hiyo, Adam Uledi mwenye mabao mawili alisema:"Japokuwa tunapitia wakati mgumu, lakini haimanishi tukate tamaa, tutaipambania nembo ya klabu ndiyo maana uwanjani tunajituma kwa bidii."
KMC iliyopo mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi tisa, katika mechi 27 imeshinda mbili, sare tatu ina mabao ya kufunga 14 na mabao ya kufungwa 47.