Msuva awatuliza mashabiki Stars

BAADA ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kutoka sare ya bao 1-1 na Sudan, mijadala mikubwa imeibuka kwa mashabiki wakihoji kama timu hiyo itatoboa kwenye michuano ya Afcon 2023, lakini mshambuliaji Saimon Msuva amewatuliza.

Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Sudan katika mchezo wa kirafiki ikijiandaa michuano ya Afcon ambapo timu hiyo imepangwa kundi F na Zambia, DR Congo na Morocco.

Mashabiki wamekuwa wakidai ikiwa Stars imetoka sare na Sudan ambao imekuwa na ligi ya kusuasua nchini kwao basi haiwezi kutoboa dhidi ya timu ilizopangwa nazo kwenye Afcon, Msuva alisema matokeo hayo

ya mchezo wa kirafiki yasiwape hofui kwani kikosi chao ni kizuri na kitafanya maajabu kwenye Afcon.

"Ule ni mchezo wa kirafiki tu na ulikuwa muhimu kutupa mazoezi mazuri lakini kocha kuangalia mapungufu ya kikosi chake na kuyafanyia kazi.

"Mashabiki wanatakiwa kukiamini kikosi chao wasiwe na hofu kabisa kwani timu hii ina wachezaji ambao walishashiriki michuano ya Afcon nikiwemo mimi, hivyo uzoefu tulionano baadhi yetu tukiunganisha nguvu na wenzetu naamini kabisa tutafanya vizuri kwenye hatua hiyo ya makundi ya michuano hiyo," alisema Msuva.

"Tunajua ugumu wa Afcon, lakini kama wachezaji tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri na kushangaza katika michuano hiyo."

Mechi za hatua ya makundi ya Afcon zitaanza Januari 13 na kumalizika Februari 11 nchini Ivory Coast na mshindi wa kwanza na wa pili kila kundi atafuzu hatua ya mtoano pamoja na timu nne zitakazomaliza na pointi nyingi zaidi kati ya makundi yote sita.