Msuva apigwa bonge la pini Difaa el Jadida

Muktasari:

Ndani ya msimu miwili ambayo ameichezea Difaa El Jadida, Msuva ameifungia klabu hiyo jumla ya mabao 24, yakiwemo 13 ya msimu uliopita upande wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.

Dar es Salaam. Ukweli umefichuka kwa mujibu wa Redio Medina FM ambayo ipo Morocco ni kwamba hakuna uwezekano wa mshambuliaji wa kimataifa wa Kitanzania, Saimon Msuva kuondoka kwenye klabu hiyo kipindi hiki cha usajili.
Licha ya uvumi kuzagaa kuwa mshambuliaji huyo yuko mbioni kutimkia Ulaya na Medina FM inadaiwa kuripoti hivyo, Difaa haipo tayari kumwachia kipindi hiki cha usajili ambacho kwa Morocco kinafungwa Septemba 19.
Kwa mujibu wa Mtanzania, anayeishi Morocco, Abdul Hamis alisema alizisikia taarifa hizo siku chache zilizopita na zikifafanua kuwa huenda Msuva akaondoka kipindi cha dirisha dogo na sio sasa.
“Kwa kuwa bado usajili upo wazi, basi tusubiri lakini kwa namna nilivyoisikia ile taarifa ni ngumu kuachiwa, anatazamwa kama mchezaji muhimu kwenye kikosi kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye msimu miwili iliyopita,” alisema Hamis.
Ndani ya msimu miwili ambayo ameichezea Difaa El Jadida, Msuva ameifungia klabu hiyo jumla ya mabao 24, yakiwemo 13 ya msimu uliopita upande wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.
Kwa mujibu wa Msuva ambaye yupo Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2019/20, alisema bado hajajua kama anaweza kuondoka au kusalia  Morocco  licha ya kukaa vikao vya hapa na pale na mabosi wa timu hiyo.
“Kabla ya kwenda Uturuki nilikaa na mabosi zangu ili kujua uwezekano wa kuondoka ulivyo, sio kama hakuna ofa ambayo imeletwa nadhani changamoto ipo kwenye maslahi.
“Nina mkataba nao, hivyo ni wazi na wao wanataka kunufaika, jambo langu ni pana kama mkataba wangu ungekuwa umemalizika nadhani ingekuwa rahisi kuondoka na nisingesafiri kwenda Uturuki,” alisema.
Msuva alisema anauheshimu mkataba wake na baada ya kurejea Morocco atakaa tena na mabosi zake ili kujua wamefikia wapi juu ya ombi lake la kutaka  kuondoka.
Inadaiwa mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga ya Ligi Kuu Tanzania Bara ana ofa ya kwenda kujiunga na miongoni mwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ na Ligi Kuu Uturuki.