Msuva apania kiatu Morocco

Muktasari:

Ndani ya misimu yake miwili akiwa na El Jadida, Msuva ambaye alijiunga na timu hiyo Julai 2017, ameifungia jumla ya mabao 24, yakiwemo 13 ya msimu uliopita.

Dar es Salaam. Nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Saimon Msuva amejiwekea malengo ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Morocco ambayo ni maarufu kama Batola Pro akiwa na klabu yake ya Difaa El Jadida msimu huu.

Msuva ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichoing’oa Burundi na kuingia hatua ya makundi ya kuwania nafasi ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, alisema ana uzoefu wa kutosha na Ligi hiyo hivyo ana kila sababu ya kutimiza ndoto yake.

“Huu utakuwa msimu wangu wa tatu kucheza Ligi ya Morocco, takribani kwenye kila msimu nilikuwa kwenye nafasi ya kuwa mfungaji bora, lakini kufanya vibaya kwa timu mwishoni mwa msimu kumekuwa kukiniangusha.

“Kama timu inapoteana ni ngumu kuendelea kufunga. Awamu hii naona kuna utofauti kuanzia kwenye maandalizi hadi kwenye aina ya wachezaji ambao wameongezwa, naamini itawezekana,” alisema mshambuliaji huyo wa pembeni.

Ndani ya misimu yake miwili akiwa na El Jadida, Msuva ambaye alijiunga na timu hiyo Julai 2017, ameifungia jumla ya mabao 24, yakiwemo 13 ya msimu uliopita.

Katika misimu yake miwili akiwa nchini Morocco, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, ameibuka kuwa mfungaji bora kwenye kila msimu kwa klabu yake ya Difaa huku pia akiwa mchezaji wa kigeni mwenye mabao mengi zaidi ndani ya misimu hiyo.

Akiwa na Yanga kabla ya kwenda Morocco, Msuva aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya misimu miwili ambayo ni 2014/15 kwa kufunga mabao 17 na 2015/16 kwa mabao 14 akilingana na Abdulraham Mussa wa Ruvu Shooting.