Mshery kupelekwa Tunisia

KIPA wa Yanga, Abuutwalib Mshery yupo nje kutokana na jeraha la goti, lakini mabosi wa klabu hiyo wamepanga kumpeleka Tunisia ili kufanyiwa upasuaji na kuruhusu areje mapema uwanjani.
Mshery aliumia goti hali iliyowafanya mabosi wa Yanga kwenye dirisha dogo la usajili  kumrejesha kwa mkopo Metacha Mnata kutoka Singida Big Stars ili kuziba nafasi yake na Mwanaspoti limedokezwa kwamba kipa huyo yupo mbioni kuondoka kwenda Tunisia  kwa matibabu zaidi.
Inaelezwa Mshery atapelekwa hospitali aliyofanyiwa upasuaji Yacouba Songne na Kibwana Shomary ambao walirejea mapema uwanjani na Daktari wa timu hiyo, Youssef Ammar ili kuthibitisha taarifa hizo alikiri kuwa na mpango wa Mshery kupata matibabu nje ya nchi.
"Kweli atafanyiwa matibabu yake nje ya nchi kule Tunisia wakati timu ikiwa inaenda kucheza mechi yake dhidi ya US Monastir," alisema kwa kifupi Ammar.
Yanga itaondoka nchini Jumanne ijayo kwa ajili ya kuwahi mchezo wa kundi D wa Kombe la  Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia utakaochezwa Februari 12 kisha ikirejea nchini itakuwa na mchezo dhidi ya TP Mazembe na baadae kuifuata Real Bamako ya Mali.
Kipa huyo alisaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Yanga baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar.