Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mserbia KenGold aanza na mambo matatu akiiwinda Yanga

KenGold Pict
KenGold Pict

Muktasari:

  • Mserbia ameanza program rasmi kikosini akiwafanyisha mazoezi mastaa wake mara mbili kwa siku kuhakikisha timu hiyo inaimarika zaidi na kuepuka kushuka daraja.

Kocha Mkuu wa KenGold, Vladislav Herić hataki kupoteza muda kwani baada ya kutambulishwa rasmi kikosini hapo, ameanza na mambo matatu kuhakikisha timu inakuwa tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.

Kocha huyo raia wa Serbia alitambilishwa juzi Jumapili Januari 19 mwaka huu kisha jana Jumatatu akaanza kazi rasmi ya kuwanoa wachezaji wakijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Yanga utakaochezwa Februari 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mserbia huyo aliyeishi zaidi Afrika Kusini, amekuja na ratiba ya kufanya mazoezi asubuhi na jioni akilenga mambo matatu ya haraka ambayo ni kupata muunganiko, fiziki na matumizi mazuri ya nafasi za kufunga.

KenGold ilianza mazoezi jana Jumatatu na kuendelea leo Jumanne, huku ikishuhudiwa nyota wa zamani wa Simba na Mwadui, Uhuru Seleman akiwa sehemu ya benchi la ufundi ikitajwa kuwa ndiye kocha wa viungo.

Katika mazoezi hayo, nyota waliosajiliwa dirisha dogo wote walikuwepo kasoro Barnard Morison pekee ambaye kutokuwepo kwake kumetajwa ni kwa sababu ya majeraha.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Heric amesema kwa sasa anasuka upya kikosi kutokana na maingizo mapya ya wachezaji akieleza kuwa anaamini hadi ligi itakapoendelea watakuwa fiti kwa mapambano.

Amesema baadhi ya mambo anayofanyia kazi ni juhudi, kasi katika sehemu za ushambuliaji na beki kuhakikisha wanaporejea katika mechi za kimashindano aone soka la ushindani na matokeo mazuri.

"Nahitaji kutengeneza muunganiko eneo la ushambuliaji, beki na timu kwa ujumla, japo ni mapema lakini naona yapo matumaini makubwa kwa kile wanachokifanya wachezaji.

"Nimeona wanatengeneza nafasi na wanazitumia, naamini kwa muda uliobaki kabla ya mechi ijayo tutakuwa sawa, mashabiki waondoe presha kwani mazuri yatakuja," amesema kocha huyo.

Nahodha wa timu hiyo, Mishamo Daud, amesema mipango na mikakati ya uongozi imeleta chachu kikosini baada ya kubaini makosa na kufanyia kazi.

Amesema ujio wa kocha mpya umeongeza nguvu na matarajio yao ni kuona wanafanya vizuri kuhakikisha timu inabaki salama Ligi Kuu akiwaomba wenzake kikosini kila mmoja kutokata tamaa.

"Hatukuwa na mwanzo mzuri lakini benchi la ufundi na uongozi wameona wapi tulikosea na kufanyia kazi, tumeona wachezaji wapya na kocha ambao kwa ujumla wameongeza chachu kikosini," amesema nahodha huyo anayecheza aneo la ushambuliaji.

KenGold ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu, imekuwa haina matokeo mazuri baada ya kucheza mechi 16 na kukusanya pointi sita ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo.