Msenegali apewa mtihani mzito
MAMBO ndiyo kwanza yanaanza Msimbazi, atakayeshindwa itakuwa imekula kwake mazima. Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr ameweka wazi jukumu zito la straika Msenegali Pape N’Daw baada ya mwezi mmoja wa kujiweka fiti.
Kerr, raia wa Uingereza alitaja jukumu hilo kuwa ni la straika huyo kuhakikisha anafunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu msimu huu na kwamba zoezi hilo anatakiwa kulianza katika mwezi mmoja ambao amempa kwa ajili ya kujiweka fiti.
“N’Daw (Pape) ni mchezaji ambaye kiufundi ni mzuri, ana mbinu na nguvu lakini anachokikosa kwa sasa ni kuwa fiti lakini tayari kocha wa viungo (Dusan Momcilovic) analifanyia kazi hilo na naamini atakapokuwa fiti ataanza kazi yake. Kimsingi nimempa mwezi mmoja na tayari amemaliza wiki.
“Ninachokitaka kwake ni kuonyesha uwezo mkubwa na kuisaidia timu ipate matokeo mazuri. Namtaka atakapomaliza muda wa kujiweka fiti aanze kazi ya kufunga mabao na nataka msimu huu afunge angalau mabao yasiyopungua 20. Hii ina maana hatakiwi kumaliza michezo miwili bila kufunga kwa sababu hiyo ndiyo kazi yake na mabao ndiyo yanayoonesha thamani yake,” alisema Kerr.
Kerr hakuishia kumnyooshea kidole N’Daw, pia amewataka mastraika wake wengine kufikia malengo kama aliyomwekea N’Daw.
“Kazi ya kufunga mabao si ya N’Daw pekee; Ajibu (Ibrahim), Mussa Hassan ‘Mgosi’, Kiiza (Hamis) na Lyanga (Danny) wanatakiwa wote kufanya kazi kama hiyo kwa kuhakikisha wanafikisha idadi ya mabao 20.
“Hakuna cha mchezaji wa kigeni au mchezaji mzawa, wote wanatakiwa kutimiza malengo niliyowawekea kwa sababu timu si ya mchezaji mmoja ni ya kila mchezaji na kila mmoja awajibike kufanya kazi yake inavyotakiwa,” alisema.