Morrison: Niombeeni

KAMA ulikuwa unadhani ni utani, soma hapa! Unambiwa leo hii Jaji Patrick Stewart, raia wa Uingereza ataisikiliza kabla ya kuitolea uamuzi kesi ya klabu ya Yanga dhidi ya Bernard Morrison, huku klabu anayoichezea kwa sasa, Simba, ikisema kesi hiyo haiwahusu, bali ni ya pande hizo mbili.

Yanga imefungua kesi namba CAS 2020/A/7397 kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) dhidi ya Morrison ambayo leo itasikilizwa na Jaji Stewart, huku Simba ikisema wanaijua kesi hiyo, lakini haiwahusu kwani inawahusisha Yanga na Morrison.

“Hata kama tunaifahamu hiyo kesi, lakini si ya klabu yetu ni ya mchezaji ndiyo sababu mpaka leo klabu haijaizungumzia,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliyekataa kutajwa jina, huku mwanasheria wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rahim Shaaban alipoulizwa kama wanafahamu chochote kuhusu kesi hiyo alisema shirikisho halifahamu.

“Taratibu za uendeshaji wa kesi kama hizo sisi huwa hautuhusu kabisa ni baina ya pande hizo mbili, ila kama tukiletewa na kufahamishwa chochote sawa, lakini mpaka sasa (jana mchana” hatujaelezwa,” alisema.

Mwanasheria wa Yanga, Simon Patrick alisema hawezi kuzungumza chochote hadi kesi hiyo itakaposikilizwa leo.

“Kwa sasa hapana, idara yangu haiwezi kusema chochote juu ya hilo hadi kesho (leo),” alisema Patrick.

Kwa upande wake, Bernard Morrisson kwenye mtandao wa Instagram aliandika "Wish me well today" akitaka wafuasi wake kumuombea na watu walimtakia heri akiwemo Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez aliyeandika 'Kila la heri'.

Awali, Yanga iliwahi kueleza kwamba Cas iliwaamuru waandae ushahidi wa kiapo cha Injinia Hersi Said na klabu imefanya hivyo na wao Yanga wataisikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao.

Yanga iliingia kwenye mgogoro na mchezaji huyo Mghana alipomaliza mkataba wake wa miezi sita na klabu hiyo kudai kumuongezea mkataba wa miaka miwili ambao Morrison aliukana.

Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF baada ya kuzisikiliza pande zote ilisema Morrison ni mchezaji huru, kwani kulikuwa na upungufu wa kimkataba na Yanga na muda mfupi baadaye alisajiliwa na Simba kwenye dirisha kubwa msimu uliopita.