Morrison: Ninaithamini Yanga kwa nafasi waliyonipa

Baada ya kuibwaga Yanga CAS, Bernard Morrison ameeleza namna anavyoithamini klabu hiyo iliyomtambulisha katika soka la Tanzania.

Morrison jana aliibwaga Yanga kwenye kesi ambayo klabu hiyo ilikata rufaa CAS ambayo ni mahakama ya usuluhishi wa kesi za michezo duniani, kupinga uamuzi ulitolewa na kamati ya sheria na hadhi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba Morrison hakuwa na mkataba na klabu hiyo wakati akijiunga na Simba.

Awali Yanga ilipinga uamuzi wa Kamati hiyo uliotolewa Agosti 12, 2020 ambao ulikuwa ukieleza kwamba Morrison hakusaini mkataba mpya na timu hiyo, ingawa ilithibitika kwamba Yanga ilimpa Dola 30,000 na kamati kuamuru mchezaji kuzirudisha fedha hizo, kabla ya Yanga kukimbilia CAS.

Jana baada ya CAS kutupilia mbali rufaa ya Yanga na kuimuru klabu hiyo kumlipa Morrison Sh 12 Milioni kama gharama za uendeshaji wa kesi, mchezaji huyo raia wa Ghana amevunja ukimya.

Katika moja ya akaunti zake za mitandao ya kijamii, Morrison amefunguka kuhusu hukumu hiyo na kubainisha kwamba hakuna kinachodumu milele.

"Kuna mwanzo na mwisho, sote tumekuwa tukingojea uamuzi huu (wema au mbaya), hatimaye umefika na umemaliza mashaka yote na mvutano.

"Nataka tu kila mtu ajue jinsi ninavyoithamini Yanga kwa nafasi waliyonipa ya kuwawakilisha na kuvaa jezi yao.

"Hakuna mtu hapa Tanzania aliyejua wala kujali kuhusu kazi yangu hadi Luc Aymael aliponileta kucheza hapa Tanzania.

"Asante Luc kwa kuniamini na kunifanya kuwa mkuu.  Kuna msemo huko kwetu Ghana kuwa "Daktari mbaya aliyekutunza hadi daktari mzuri alipofika lazima athaminiwe".

"Hata kama alikuwa mbaya, alikuweka hai mpaka yule bora alipofika, nasema rasmi asante kwa Yanga SC na yeyote aliyenifanya nitabasamu au kunipenda nirudi klabuni kwao, bila kusahau mapenzi niliyoonyeshwa na mashabiki wao," alimaliza Morrison.