Morrison aishinda Yanga CAS

MAHAKAMA ya usuluhishi wa kesi za michezo Duniani (CAS) imetupilia mbali rufaa ya Yanga ya kupinga uamuzi uliotolewa na kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kwamba  mchezaji wa kimataifa wa Ghana, Bernard Morrison hakuwa na mkataba nao kipindi anajiunga na Simba.
Yanga ilipinga uamuzi wa kamati hiyo ya TFF uliotolewa Agosti, 12,  2020  ambao ulikuwa ukieleza kwamba Morrison hakusaini nao mkataba ingawa ilithibitika kwamba Yanga ilimpa Dola 30,000 ambazo kamati ilimuamuru mchezaji huyo airudishie Yanga.
Kamati hiyo ilidai mkataba wa  Morrison ulimalizika Julai, 14,  2020. Hivyo kuanzia hapo alikuwa huru na mkataba wa mara ya pili wa Yanga haukuwa unatambulika.
Yanga ilipinga uamuzi huo wa TFF na kukata rufaa kwenda CAS wakiomba uhalali wa mkataba waliodai kwamba wamemsainisha kwa mara yapili na Morrison aamrishwe kulipa Dola 200,000 kama adhabu ya kusaini mkataba na Simba wakati bado alikuwa na mkataba na Yanga.
Baada ya rufaa  hiyo CAS kupitia taarifa yake iliyotoa leo imefafanua kwamba ilikaa kikao kwa njia ya video Julai mwaka huu na baada ya majadiliano imefikia uamuzi wa kuitulipilia mbali rufaa hiyo iliyowasilishwa na Yanga.