Yanga kumlipa Sh12 milioni Morrison

Kiungo wa Simba, Bernard Morrison atalipwa kitita cha Swis 5,000 (sawa na Sh12,396,787) baada ya kushinda kesi iliyokuwepo baina yake na Yanga.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Novemba 22, 201 na Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) ikisainiwa na msimamizi wa shitaka hilo, Patrick Stewart, ambayo pia iliambatana na Yanga kulipa asilimia 90 za uendeshwaji wa shauri hilo.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa leo, imeeleza kuwa ushahidi uliotolewa na Yanga juu ya mkataba mpya uliotolewa na Yanga ulikuwa na makosa mengi na kushindwa kuwa na ushahidi wa kutosha kama ulisainiwa na Morrison.

Hukumu hiyo ya Cas ilisema shauri lililofunguliwa na Yanga Agosti 27, 2020 dhidi ya uamuzi wa  Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetupwa.

CAS ilisema kuwa uamuzi wote uliotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF wa 12 Agosti 2020 unabaki kama ulivyo.

Katika hukumu hiyo iliyokuwa na kurasa 29, ilisema pia madai yote aliyoyataka kiungo huyo raia wa Ghana hayana msingi na hayakubaliki.