Morrison, Kagere waanzia nje

Saturday December 05 2020
simba pic
By Mwandishi Wetu

KAMA ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza wa ugenini dhidi ya Plateau United, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amewaanzisha benchi washambuliaji, Meddie Kagere na Bernard Morrison, huku beki wa kati Mkenya, Joash Onyango akikosekana kabisa katika mechi yao ya leo.
Simba inaikaribisha Plateua katika mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ambao kwa sasa umeanza kupendeza saa chache kabla ya kuanza hapo saa 11 jioni.
Kocha Sven amekianzisha kikosi kama kilichoanza ugenini mjini Jos, Nigeria na kushinda bao 1-0, ukimuondoa Joash ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mzamiru Yasin aliyeanza kikosi cha kwanza sambamba na Jonas Mkude eneo la kati, huku Erasto Nyoni aliyeanz amchezo uliopita kama kiungo mshambuliaji akirudishwa kuziba nafasi hiyo ya Joash.
Kikosi kizima kilichoanza ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Erasto Nyoni, Pascal Wawa kwenye eneo la ulinzi wakisaidiwa na Mkude, huku winga wa kulia ni Hassan Dilunga, huku Mzamiru akicheza kama kiungo mshambuliaji na Nahodha John Bocco ndiye straika, huku akipigwa tafu na Clatous Chama na Luis Miquissone.
Kwa aina ya kikosi kilichoanza ni wazi Sven anaendelea kutumia mfumo wa 4-3-2-1 na anaweza kubadilisha ndani ya uwanja na kuwa 4-3-3.

Advertisement