MONJA: Babu katika ubora wake
Muktasari:
Yanga imetinga 1998 na Simba 2003. Yanga kwenye kundi lake haikushinda mechi hata moja kati ya mechi sita ilizocheza kwani ilipoteza mechi nne na sare mbili. Simba kwenye kundi lake 2003 ilishinda mechi mbili, ikapoteza tatu na sare moja. Hayo yalijiri tangu Monja alipoanza soka mpaka sasa anafikiria kustaafu.
KUNA kitu kimoja ambacho inawezekana umekisahau.Katika miaka 22 iliyopita ambayo straika mkongwe, Monja Liseki amecheza soka Simba na Yanga zimetinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja tu kila moja.
Yanga imetinga 1998 na Simba 2003. Yanga kwenye kundi lake haikushinda mechi hata moja kati ya mechi sita ilizocheza kwani ilipoteza mechi nne na sare mbili. Simba kwenye kundi lake 2003 ilishinda mechi mbili, ikapoteza tatu na sare moja. Hayo yalijiri tangu Monja alipoanza soka mpaka sasa anafikiria kustaafu.
Amecheza Simba na Yanga msimu mmoja wa 1997/98. Alisajiliwa na Simba lakini Yanga wakamuomba kwa mkopo awasaidie kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezaji huyo ambaye kwa sasa anaichezea Mwadui ya Shinyanga iliyopanda daraja hadi Ligi Kuu Bara, anaingia mwaka wa 22 akiwa anacheza mpira wa ushindani tangu alipoanza kucheza mechi za Ligi Kuu Bara akiwa na Sigara ya Dar es Salaam mwaka 1993.
Huu ni mwaka wake wa 38 tangu alipozaliwa, Agosti 8, 1977 umri ambao kwa mchezaji ni mkubwa, lakini kwake ni historia. Kwa sasa ni maarufu kwa jina la Babu Monja na wanapomwita, mwenyewe anawaitikia wajukuu maisha yanaendelea.
Lakini huo ndiyo ukweli wa mambo kwa sababu ya umri huo alionao kwa mchezaji wa ndani ni wachache kuufikia wakiwa katika maisha ya mpira, hivyo Monja ana kila sababu ya kujidai.
Kwani unapomtazama sasa uwanjani, yuko katika ubora wake uleule, nguvu, kufunga na akili ya mpira, ukimwona anafurahisha. Ni vigumu kuwakuta wachezaji wa umri wake wanaocheza nafasi za ndani kama yake ya straika uwanjani, wakiwa katika ubora wao labda kwa makipa tu.
Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ndiye aliyeamua kumrudisha Monja uwanjani baada ya kumwona yuko vizuri ili waipandishe daraja. Kwani mbali na ubora wake uwanjani, ni mlezi kwa wachezaji wenzake ambao katika kikosi hicho, anawazidi mbali kwa umri.
Tena anafurahisha zaidi pale anapowaita wajuu zake na yeye wanamwita Babu Monja.
Siri ya ubora wake
Wachezaji wengi wanashindwa kutambua thamani zao kwa sababu hawajitambui, achana na kitu kinaitwa starehe ni nzuri lakini ndiyo kimekuwa kikiwaharibia wengi.
Monja anasema, anaamini anaweza kufanya mambo makubwa zaidi licha ya kuwa umri wake umekwenda kwa sababu kimwili yuko vizuri na akatolea mfano wa Madaraka Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio’ aliyestaafu kucheza soka na miaka 41.
Monja amekwenda mbali na kusema: “Kingine huwa nafanya sana mazoezi na kujipa muda mrefu wa kupumzika pamoja na kula vizuri.”
Aitaka Ligi Kuu, afundishe
soka vijana
Monja anasema, hana ndoto za kuwa kocha wa mpira kwa sababu hapendi. Lakini atawafundisha vijana kutokana na kiwango chake atakachokuwa anawaonyesha uwanjani na ndiyo maana, baada ya Mwadui kupanda Ligi Kuu anataka kuucheza msimu ujao tu.
“Bado niko vizuri na baada ya kupanda, nataka msimu huu tuliopanda, nicheze Ligi Kuu niwaonyeshe vijana soka linachezwaje uwanjani,” anasema Monja.
“Sina ndoto za kuwa kocha kwa sababu sipendi, nitawaelekeza tu kama mkubwa wao na mambo mengine.”
Maisha ya Mwadui
Monja anasema, maisha ya Mwadui ni mazuri kwa sababu wanaishi kama familia moja.
“Maisha ya Mwadui ni mazuri kwa sababu wote tunaishi kama familia moja tuliokuwa na lengo moja na ndiyo maana hata tukafanikiwa,” anasema Monja.
“Kama ulivyoona ligi ilikuwa ngumu sana, haikuwa rahisi kupanda, lakini tulipambana tukafanikiwa.”
Kero kwa mastraika
Sehemu kubwa ya makocha wa timu za Ligi Kuu kero yao imekuwa kwa washambuliaji hawafungi na wanaotamba ni wageni kutoka nje ya nchi. “Sababu kubwa ni kukosa utulivu, huwa wanaurupuka lakini wakijifunza kutulia kila kitu kitakwenda sawa. Makocha nao waamini, unaposhindwa kumwamini mchezaji naye anacheza hajiamini matokeo yake anaharibu kila kitu,” anaeleza Monja na kumtolea mfano Said Bahanuzi ambaye alishindwa kutamba kwenye kikosi cha Yanga lakini sasa amekuwa lulu kwa maafande wa Polisi Morogoro.
Akumbuka pikipiki ya Mtibwa
Monja anakumbuka matukio mengi lakini lililowahi kumtokea Mtibwa mwaka 2004-2005 chini ya Kocha Mkenya Twahir Muhiddin ndilo analikumbuka sana.
Anasema, walikuwa katika maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu moja ya Madagascar wao walikuwa wanasafiri. Yeye na Alphonce Modest walichukua pikipiki ya bosi wao, Ally Karuma wakapakizana kwa ajili ya kujiburudisha. Dereva alikuwa Modest lakini kilichokuja kutokea, pikipiki iliwadondosha wakaumia.
“Kila ninapokumbuka tukio hilo, huwa inaniuma sana, kwani baada ya kudondoka tuliumia kidogo, tulipata michubuko ya hapa na pale na mwalimu Twahir alipogundua, alituacha kwenye safari ya Madagascar, tukabaki kambini Mtibwa.”
Monja ameshazichezea timu mbalimbali kama, Mtibwa miaka 15, Sigara miaka mitatu, Simba na Yanga mwaka mmoja, Miembeni ya Zanzibar mwaka mmoja.
Monja alicheza msimu mmoja kwa timu mbili ya Simba na Yanga mwaka 1997-1998. Katika msimu huo, aliichezea Simba mechi za ligi na baadaye Yanga walimchukua kwa mkopo ili awasaidie mashindano ya Kimataifa walipokuwa wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Anaitaja Mtibwa kuwa ni nyumbani kwake kwa sababu ndiyo alidumu nayo kwa miaka mingi. : “Sina ushabiki wa Simba wala Yanga licha ya kuwa nilizichezea kwa nyakati tofauti. Naweza kusema, Mtibwa ndiyo kila kitu kwa sababu ndiyo nilidumu nayo kwa muda mrefu, miaka 15 ni mingi.”
Mafanikio: “Naweza kusema, mpira umenipa mafanikio kwa sababu hadi leo naendesha familia yangu bila matatizo.Siwezi kuorozesha vyote.”
Kilichomstaafisha awali
Monja anasema, aliamua kupumzika baada ya kutoka Zanzibar alikokuwa anaichezea Miembeni ambayo ilimwomba kutoka Mtibwa ili wakaipandishe ndipo alipofuatwa na Julio ili wakaipandishe Mwadui.