Prime
Moallin afichua hesabu mpya Yanga, akiwataja Dube, Depu
YANGA imereja nyumbani ikianza hesabu mpya za kuwafuata Fountain Gate sasa kocha wao wa muda kuna mambo mawili ameyatangaza akianza na mpango wa mechi nne zilizosalia lakini akafunguka juu ya mastraika wake wawili.
Yanga juzi ilishinda ugenini dhidi ya Mashujaa, ikiichapa kwa mabao 2-0, bingwa huyo mtetezi akiendelea kukaa juu ya msimamo akiisikilizia Simba iliyokuwa uwanja wa nyumbani jaa dhidi ya Pamba Jiji, wekundu hao ikiendelea kulifukuzia taji la Ligi Kuu Bara.
Yanga baada ya mchezo wa Mashujaa, itawafuata Fountain Gate kwenye mchezo mwingine wa ugenini Juni 18, pale Uwanja wa Sheikh Amri Abed, jijini Arusha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Moalin alisema wakati kikosi hicho kikibakiza mechi nne kumaliza msimu wa ligi, hesabu zao kwa sasa ni kuchukua mpango wa mchezo mmoja kwenda mwingine ili kujipunguzia presha ya matokeo.
Moalin alisema Yanga ina faida ya kuwa na mtaji wa pointi ikitofautiana kwa pointi mbili dhidi ya Simba waliopo nafasi ya pili, ambapo hataki wachezaji wake wacheze kwa kufikiria timu inazozifukuza zaidi a kuangalia mchezo ulio mbele yao.
“Ligi ipo kwenye mbio kali na tupo juu ya msimamo, tunaongoza kwa pointi zipo timu zinatufukuza kwa karibu, tunachofanya sasa kama mpango wetu ni kutozingatia hayo yote tunatakiwa kuwa makini na kila dakika 90 zilizo mbele yetu.
Moalin aliongeza kuwa anafurahishwa na ukomavu ambao wachezaji wake wanaonyesha ambapo imehakikisha mabao yanapatikana huku ikiwa imara kwenye eneo la ulinzi kutoruhusu bao lolote.
“Ndio nafurahia nidhamu ya wachezaji wetu, angalia kitu kuhimu ambacho kitaamua mechi zetu ni kupata mabao, tumekuwa tunatengeneza nafasi na kuzitumia, unaposhinda kwa kupata mabao mawili kwenye uwanja mgumu kama ule ni kitu kizuri.
“Ukiondoa kufunga eneo la kiungo nalo tumekuwa imara sana, tumeweza kutegua mitego yote ya wapinzani lakin kule nyuma nako kumeimarika, tunatakiwa kuendelea kwa kutoruhusu bao ili tuwe salama.
DUBE, DEPU SUALA LA MUDA
Washambuliaji wawili wa Yanga wamemaliza dakika 90 zingine bila bao ambapo Moalin akasema bado wawili hao wana umuhimu mkubwa kwenye kikosi hicho ambapo suala la kufunga litakuja taratibu.
“Nafahamu kwamba hawajafunga lakini kuna umuhimu wao mkubwa sana kwenye timu yetu, angalia Dube jana (juzi) ametengeneza nafasi ya kufunga kwa Mudathir (Yahya) lakini hata Depu alikuwa na hesabu nzuri alipoingia.
“Kama ambavyo nasema kila wakati kuna wakati mchezaji au mshambuliaji anapitia ukame wa namna hii lakini kitu muhimu ni juhudi zao ambazo wamekuwa wanazionyesha uwanjani, wana umuhimu mkubwa kwenye kikosi chetu.