MO Dewji atoa kauli nzito Simba kupelekwa Zanzibar

Muktasari:
- Simba inatarajiwa kurudiana na RS Berkane ya Morocco Jumapili ya Mei 25 baada ya awali kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane.
RAIS wa klabu ya Simba, Mohamed 'MO' Dewji, ametoa kauli nzito kuhusiana na mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kupelekwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, humu akiwahamasisha wanasimba kwamba mnyama atanguruma popote na Jumapili itabeba ndoo.
Simba inatarajiwa kurudiana na RS Berkane ya Morocco Jumapili ya Mei 25 baada ya awali kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane.

Hata hivyo, kupelekwa kwa mchezo huo wa marudiano visiwani Zanzibar, umeonekana kumtibua Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mo Dewji ambapo mapema leo ametoa waraka akionekana kuhisi Simba ni kama imeonewa kuhamishwa kutoka Benjamin Mkapa.
Kupitia taarifa aliyoiweka katika mtandao wa kijamii wa Instagram Mo Dewji alisema hawakwenda Zanzibar kwa hiari yao bali wanatimiza wajibu.
"Sisi Simba kucheza New Amaan Complex kwa mtazamo wangu binafsi hatukutendewa haki, Tunaenda Zanzibar si kwa hiari yetu bali kwa wajibu na tutatimiza wajibu huo," ilisema taarifa hiyo na kuongeza;
"Kwa wachezaji wetu mnaovaa nembo yenye historia ingieni New Amaan vichwa juu chezeni kwa ujasiri kwa umakini na kwa utulivu kama mashujaa wa Simba mlivyo."

Taarifa hiyo imeongeza; "Kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa, kila hatua ya ukarabati wa uwanja ilifuatwa kwa makini ili kuhakikisha unakuwa tayari kwa mechi hiyo ya fainali. Wakati huohuo, baadhi ya matukio yaliyotokea nyuma ya pazia yameacha maswali ya msingi, Taarifa zilianza kusambaa mtandaoni kabla ya taarifa rasmi kutolewa, tulieleza wasiwasi wetu kwa wazi.
"Pamoja na juhudi hizi zote, CAF imethibitisha kuendeleza uamuzi wa kuhamishia fainali hiyo Zanzibar, bila shaka, matokeo haya ni ya kusikitisha si kwa Simba tu, bali kwa mashabiki wetu, na kwa wote waliotoa juhudi kubwa kuandaa tukio hili katika historia ya Simba na Tanzania."
“Kwa mazamo wangu wa kibinafsi, hatukutendewa haki."

Taarifa hiyo imefafanua, na ikiwa imetolewa saa chache kabla ya mechi hiyo kupigwa Jumapili na tayari Wekundu hao wameshatimba visiwani humo tangu jana tayari kujiandaa na mchezo huo.
Hii ni fainali ya pili kwa Simba kucheza fainali ya CAF, kwani mwaka 1993 ilitinga fainali ya Kombe la CAF na kupoteza mbele ya Stella Abdijan ya Ivory Coast, lakini ni mara ya tatu kwa timu za Tanzania kufika hatua hiyo, kwani Yanga ilicheza fainali ya KOmbe la Shirikisho 2022-2023 na kupoteza kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo kuwa sare ya 2-2.