Mnyama kapigwa hukoo, Mbeya City yavunja rekodi

Monday January 17 2022
FULL PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Licha ya kucheza pungufu lakini Mbeya City imekomaa na kuvunja uteja kwa kuilaza Simba bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa katika uwanja wa Sokoine jijini hapa.

 Mbali na kuvunja uteja, City wanaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Ligi Kuu kuwafunga Simba ambao walikuwa wamecheza mechi 10 bila kupoteza hata moja.

Ikicheza kwa jitihadi, umakini na kujiamini, Mbeya City ilionesha soka safi na kuweza kudhibiti wapinzani hao ambao walikuwa wa moto kusaka mabao.

Hata hivyo Simba watajilaumu kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi ambazo zingeweza kuwanufaisha kuondoka na alama tatu, kwani mbali na kutotumia vyema nafasi hizo, lakini walikosa mkwaju wa penalti ambao Chris Mugalu alishindwa kufunga baada ya shuti lake kugonga nguzo.

Kabla ya kukosa penalti hiyo, Mugalu alikuwa amefunga bao dakika ya pili lakini iliamuliwa kuwa ameotea alipopokea mpira wa faulo wa Benard Morrison.

Ilikuwa dakika 20 ambapo Straika, Paul Nonga alipoiandikia bao akipokea pasi ya Juma Luizio na kuweza kuwapita mabeki hadi kumpunguza Aish Manula na kuukwamisha mpira wavuni.

Advertisement

Dakika ya 43 Beki wa Mbeya City, Mpoki Mwakinyuke alijikuta akila umeme baada ya kumchezea rafu, Mugalu ambapo mwamuzi Raphael Ikombi (Morogoro) alimuonesha kadi nyekundu.

Hata hivyo Simba walionekana kupambana kwani dakika ya 90, Meddie Kagere aliweza kuweka mpira wavuni kwa kichwa akipokea mpira wa Morrison lakini mwamuzi wa pembeni, Leonard Mkwambo aliashiria mfungaji kuwa ameotea.

Hadi dakika 90, Simba iliondoka vichwa chini kwa kukosa kitu katika Uwanja huo, huku wenyeji wakibaki na shangwe kwa ushindi huo ambao unaifikisha pointi 19 na kupanda nafasi ya tatu baada ya mechi 12.

Advertisement