Mnoga amaliza kibabe chama jipya la Beckham

Muktasari:
- Huu ni msimu wa kwanza kwa beki huyo wa timu ya taifa 'Taifa Stars' kuitumikia timu hiyo akitokea Aldershot aliyeichezea kwa misimu miwili.
BEKI wa Kitanzania, Haji Mnoga anayekipiga Salford City ya England amemaliza kibabe msimu akifunga bao moja na asisti nne.
Huu ni msimu wa kwanza kwa beki huyo wa timu ya taifa 'Taifa Stars' kuitumikia timu hiyo akitokea Aldershot aliyeichezea kwa misimu miwili.
Mnoga alicheza mechi 39 kati ya 46 za timu hiyo kwa dakika 3306 na amekuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi hicho na kuwaweka benchi nyota mbalimbali wa eneo hilo.
Ligi ya nchi hiyo imetamatika na Salford ambayo kwa sasa inamilikiwa na nyota wa zamani wa Manchester United, David Beckham na Garry Naville imemaliza nafasi ya nane kwenye mechi 46 imeshinda 18, sare 15 na kupoteza 13 ikusanya pointi 69.
Hata hivyo mkataba wa beki huyo umalizikia mwishoni mwa mwezi Mei na ilielezwa viongozi tayari wameanza mazungumzo ya kumuongezea mpya ili aendelee kusalia kikosini hapo.
Mnoga huenda akaendelea kuichezea timu hiyo msimu ujao hasa baada ya kumilikiwa na nyota hao wa zamani ambao wamesema lengo lao ni kuhakikisha inapanda hadi Ligi Kuu England kutoka League Two iliyopo sasa.