Mnigeria anakula mkataba Simba

INGAWA mabosi wa Simba wanakuna vichwa juu ya uamuzi wa kumsajili kiungo, Mnigeria Udoh Etop aliyepo kwenye majaribio lakini kuna kila dalili kwamba zali litamuangukia baada ya viongozi kumkosa Msenegali waliyekuwa wanamnyatia Morocco.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alitoa mapendekezo ya kuongezewa straika mmoja na walikuwa tayari wamempata raia wa Senegal anayecheza soka la kulipwa Morocco ila upatikanaje wake umekuwa mgumu na ameshacheza michuno ya kimataifa.

Kura sasa zimemdondokea kiungo, Udoh na mabosi wa Simba wamemueleza wapo tayari kumpatia mkataba wa miezi sita kutokana na kiwango bora alichoonyesha.

Udoh aliyeonyesha kiwango bora kwenye kombe la Mapinduzi ameambiwa kama atakuwa tayari kusaini mkataba mkataba wa miezi sita bila ya pesa ya usajili pamoja na kulipwa Dola 3,000 zaidi ya Sh6 milioni kila mwisho wa mwezi wapo tayari.

Inaelezwa kwa upande wa Udoh mwenyewe amewambia Simba apewe Dola 18,000 zaidi ya Sh32 milioni na mshahara wa Dola 5,000 zaidi ya Sh10 milioni yupo tayari kusaini.

Kwahiyo kuna mvutano mkubwa kati ya pande zote mbili ili kukubaliana na suala hilo na kufanya uamuzi kabla ya dirisha kufungwa Udoh kusaini au watashindwana.

Katika hatua nyingine wakala wa mchezaji huyo tayari amewasili Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kusimamia suala hilo la Udoh na kuona kama watakubaliana au hatakubali kushusha maslahi yake.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema maamuzi katika masuala yote ya usajili wamemuachia kocha wao Pablo.

“Jambo lolote kwenye usajili ndani ya timu yetu Pablo ndio mwenye maamuzi ya mwisho ila ambacho nawaeleza wapenzi wa Simba tutafunga dirisha hili la usajili kwa kishindo kikubwa,” alisema Try Again.

Kama Simba watamshusha Clatous Chama ataingia nafasi iliyoachwa wazi wa Dancun Nyoni huku Udoh italazimika Simba kuachana au kumtoa kwa mkopo nyota mmoja wa kigeni ndani ya kikosi chao ambaye anatajwa kuwa ni Paschal Wawa.