Mmanga: Hata mimi huwa sielewi kabisa napata kadi nyekundu

BEKI na nahodha wa Polisi Tanzania, Mohamed Mmanga amesema kinachotokea juu ya kadi nyekundu anazopata hata yeye binafsi hakielewi.

Kauli ya Mmanga inajiri baada ya nyota huyo kupata tena kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting huku akishuhudia kikosi chao kikipoteza kwa kufungwa bao 1-0, mechi iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Uhuru.

Wakati Ligi hiyo ikiwa mzunguko wa nne tayari nyota huyo ana nyekundu mbili baada ya kupata dhidi ya Yanga kwenye mechi ya kwanza tu ya ufunguzi iliyopigwa Agosti 16 na Polisi Tanzania kupoteza mabao 2-1.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Mmanga alisema ni jambo linalomuumiza huku akikiri hujikuta akifanya hivyo pasipo kukusudia.

“Kuna muda najiona nafanya sahihi kumbe ninaigharimu timu, binafsi niombe radhi viongozi na benchi la ufundi kwa kilichotokea kwani mimi ni binadamu na ni kijana ninayejifunza kila siku kutokana na makosa,” alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa kikosi hicho Mrundi, Joslin Bipfubusa alisema licha ya yote ila bado ana imani kubwa na nyota huyo katika timu yake hivyo atakachokifanya ni kukaa naye chini ili kumjenga tu kisaikolojia.

Kadi hiyo inakuwa ni ya tatu kwa Mmanga katika karia yake ya soka baada ya awali kupata wakati akiichezea Jamhuri ya kwao Visiwani Zanzibar msimu wa 2012/2013, kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Falcon FC.