Mlandege yageukia Ligi Kuu

Muktasari:
- Mlandege iliitoa Kikungwi Stars kwa penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kuungana na KMKM, Mafunzo na Malindi kwa Ukanda wa Unguja, huku kwa Pemba zilizopenya ni Chipukizi ambao ni watetezi wa taji hilo, Junguni United, Mwenge na Super Falcon.
BAADA ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup), Mlandege inarejea tena uwanjani leo katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) na jana Ijumaa iliikaribisha Mwembe Makumbi inayoongoza msimamo wa ligi hiyo.
Mlandege iliitoa Kikungwi Stars kwa penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kuungana na KMKM, Mafunzo na Malindi kwa Ukanda wa Unguja, huku kwa Pemba zilizopenya ni Chipukizi ambao ni watetezi wa taji hilo, Junguni United, Mwenge na Super Falcon.
Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi, itaikaribisha Mwembe Makumbi kwenye Uwanja wa Mao A mjini Unguja, wakati kwenye Uwanja wa Gombani, Chipukizi itakwaruzana na Mwenge, mechi zote zikipigwa kuanza saa 10: jioni.
Mlandege ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 41, nne pungufu na ilizonazo Mwembe Makumbi inayoongoza ikiwa ni moja ya kati ya timu nne zilizopanda daraja msimu huu sambamba na Junguni, Tekeleza na Inter Zanzibar na ushindi dhidi ya wababe hao ifarikisha alama 44.
Makocha wa timu hizo wametambiana wakirejea matokeo ya mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba 21 mwaka jana na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, lakini wakipigia hesabu kubeba ubingwa kwa msimu huu, taji linaloshikiliwa kwa sasa na JKU iliypo nafasi ya tano ikiwa na pointi 37.
Mwembe Makumbi katika mechi 22 ilizocheza hadi sasa imeshinda 13, mbili zaidi na ilizoshinda Mlandege, lakini imetoka sare sita na kupoteza tatu, ikifunga mabao 33 na kufungwa 16, wakati wenyeji wao wametoka sare nane na kupoteza tatu pia, ikifunga mabao 40 na kufungwa 15, hali inayofanya mechi ya leo kuwa ngumu na kutolewa macho na mashabiki wengi wa soka wa Zanzibar.
Kwa mechi ya Gombani, Chipukizi iliyopo nafasui ya 11 inakwaruzana na Mwenge inayoshika nafasi ya 11 zote zikiwa na mtihani wa kusaka pointi tayu ili kujiweka eneo zuri dhidi ya janga la kushuka daraja.
Chipukizi ina pointi 28 kutokana na mechi 22, wakati Mwenge ina alama 21 kupitia mechi 21, kitu kinafanya pambano hilo kuwa lina ugumu kwa timu zote.
Kwa sasa Tekeleza ndio inayoburuta mkia katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi tatu tu kupitia mechi 22, ikiwa ndiyo pekee haijaonja ushindi wa katika ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Inter Zanzibar yenye pointi tano kwa sasa zikiwa ndizo zipo katika hatari kubwa ya kushuka daraja kurudi zilipotoka.