Mkwasa asaka mrithi wa Edward Manyama

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa amesema amekabidhi ripoti kwa uongozi wa timu hiyo na kuonyesha nafasi sita za usajili ikiwemo mrithi wa Edward Manyama aliyekuwa beki wao wa kushoto aliyehamia Azam FC na kuwaachia pengo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Mkwasa aliliambia Mwanaspoti, licha ya timu hiyo kuwa na mahitaji makubwa ya kukiboresha hicho ila ataanza na nafasi ya beki wa kushoto kutokana na uhitaji mkubwa wa timu hiyo kuelekea msimu ujao baada ya kuondoka kwa Manyama.

“Tuna mahitaji mengi katika kikosi chetu ukiangalia msimu uliomalizika tulishindwa kufikia malengo ya kumaliza nafasi nne za juu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara kwa wachezaji wangu, hivyo kwa msimu ujao hatutaki tena hilo likijirudia” alisema.

Aidha alisema ameshatoa ripoti yake ya usajili kwa uongozi akihitaji kufanyia marekebisho eneo la kipa na maeneo mengine ili kutengeneza upana mkubwa wa kikosi kuelekea msimu ujao ambao anaamini utakuwa ni mgumu zaidi ya ulioisha.

“Msimu huu hatujafikia malengo ambayo yalikuwa ni kumaliza ndani ya nne bora sababu kubwa ni kutokana na majeruhi ambayo yalituandama, sasa nimeeleza uongozi wangu kupitia ripoti yangu kusajili wachezaji ambao wataleta ushindani na kuwepo na kikosi kipana kitakachotusaidia kuleta ushindani mkubwa kwa timu 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu kwa msimu ujao,” alisema.

Katika hatua nyingine Mkwasa alisema katika usajili watazingatia zaidi umakini kuleta wachezaji watakaokuwa msaada mkubwa wa timu hiyo ya kutimiza malengo yao ya msimu ujao.

“Hatuna muda mrefu na hii ni kutokana na ligi kutarajiwa kuanza Septemba, hivyo tunataka kufanya kila kitu mapema, kusajili wachezaji wazuri na kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao.”