Mkude ni yule yule

Saturday January 15 2022
Mkude PIC

Kiungo wa Simba Jonas Mkude, katikati ya Khalid Aucho na Feisal Salum wa Yanga akitoa pasi katika mchezo wa Kariakoo Derby iliyochezwa jana katika Uwanjan wa Benjamini Mkapa.

By Mwanahiba Richard

KIUNGO Jonas Mkude amesema moto wake uwanjani ni uleule hata kama amekuwa akiwekwa nje kupisha wenzake kucheza na kwamba anafurahi kuendelea kubaki kwenye kiwango chake.

Mkude, alikuwa akipigishwa benchi na Mganda, Taddeo Lwanga ambaye kwa sasa ameumia goti na kumfanya mchezaji huyo mwandamizi wa kikosi cha Simba kupewa nafasi ya kucheza na kuonyesha kiwango kikubwa kilichomvutia hadi Kocha Mkuu, Pablo Franco.

Akizungumza kisiwani hapa Mkude alisema, yeye ni mchezaji na kazi yake ni kucheza mpira hivyo hajawahi kukata tamaa hata anapokuwa nje ya uwanja kwa kukosa nafasi bali huamini kuwa kuna siku atacheza.

“Kwa ufupi hii ni kazi yangu na hata nikae nje kwa kipindi kirefu hakunizuii kucheza katika kiwango bora maana hii ndiyo kazi yangu, kikubwa ni kujituma mazoezini na kufuata kile unachoelekezwa, ndiyo njia sahihi kwa mchezaji ili kuisaidia timu kufikia malengo yake.”

Kuhusu kuelekea mechi zao za kimataifa za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Mkude alisema lengo lao ni kufika mbali zaidi.

“Halafu watu wasiniangalie mimi kama mimi kuwa nafanya nini ndani ya Simba, wachezaji wote tuna ushirikiano mzuri ndio maana tunafanya vyema kwenye mashindano yote, kila mtu ajitoe kwa ajili ya timu,” alisema Mkude, Mchezaji Bora wa Desemba katika tuzo zinazotolewa na wadhamini wa Simba, Emirate Alluminium akiwazidi Joash Onyango na Henock Inonga.

Advertisement


Advertisement