MKONGO WA SIMBA AITAKA YANGA

Sunday August 02 2020
MKONGO PIC

DIRISHA la usajili kwa msimu mpya wa 2020-2021 umefunguliwa rasmi jana, huku Simba, Yanga na Azam zikiwa zimeshaanza vita mapema ya kusajili mashine mpya, lakini unaambiwa straika matata kutoka DR Congo aliyekuwa akiwindwa na Simba, fasta amebadili upepo na kujipeleka Yanga.

Wekundu wa Msimbazi, waliwahi kumuwinda straika huyo wa AS Vita, Makusu Mundele kabla ya kumpotezea, lakini sasa jana amefichua safari yake ya kuanza kuja kucheza Tanzania akiifikiria Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Mundele amefichua kocha wake, Florent Ibenge alimfuata na kumuuliza kama yuko tayari kucheza soka Tanzania na hasa Yanga.

Mundele alisema Ibenge amemweleza juu ya Yanga kutafuta straika mfungaji na kwake amemshauri kujiunga na timu hiyo.

“Ameniita Kocha Florent (Ibenge) akaniuliza kama nitakuwa tayari kucheza Tanzania, nikamweleza niliwahi kupata ofa ya Simba, lakini juu ya Yanga nilimjulisha hawakuwahi kunifuata,” alisema Mundele na kuongeza;.

“Ameniambia kama nitakuwa tayari nimwambie haraka ili aniunganishe na bosi mkuu wa Yanga ili azungumze na mimi nitamjibu.”

Advertisement

Aidha Mundele ameongeza katika mazungumzo yake na Ibenge amemweleza juu ya mastaa wawili ya Vita kiungo Mukoko Tonombe na winga Tuisila Kisinda wakati wowote wataungana na kikosi hicho cha Jangwani kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano mingine.

“Ameniambia Kisinda (Tuisila) na Mukoko (Tonombe) wamesajiliwa na Yanga na wakati wowote wataungana na timu hiyo. Hawa ni wachezaji bora hapa Vita naona hiyo timu itakuwa na wachezaji wazuri sana ngoja nitakwambia nitakachomjibu kocha Jumatatu,” alisema Mundele.

Akizungumzia kurejea kwake baada ya kuvunjika mguu, Mundele alisema kwa sasa ameshapona kabisa na ameshaanza kujifua kwa mazoezi makali na kikosi cha Vita kinachotaka kuanza maandalizi ya msimu mpya.

“Mpaka sasa kuumia kwangu ilikuwa kama miujiza, ila nashukuru kwa sasa nimepona kabisa na nimerudi kazini, madaktari walinipa ruhusa ya kufanya mazoezi makali na sasa nasubiri kuanza maandalizi ya msimu.”

SHIKHALO AMFICHUA WERRE

Katika hatua nyingine, kipa wa Yanga Mkenya Farouk Shikhalo amesema mshambuliaji Jesse Werre yuko tayari kuja Yanga kama mabosi wa klabu hiyo watamhitaji.

Akizungumza na Mwanaspoti Shikhalo alisema amelazimika kumpigia simu Werre kisha kumuuliza kama ni kweli anakuja Yanga.

“Niliona hizi taarifa kupitia mitandao hapa nikashtuka nilipompigia kumuuliza akaniambia bado hajazungumza na kiongozi yoyote wa Yanga,” alisema Shikhalo.

Shikhalo alisema ingawa Werre bado hajafuatwa rasmi na Yanga, lakini amemweleza yuko tayari kuja Yanga endapo watamshawishi na dau zuri.

Alisema kwa changamoto alizoziona katika safu yao ya ushambuliaji kama kweli mabosi wa Yanga wanamtaka mshambuliaji huyo basi ni hatua nzuri na ataisaidia timu hiyo.

“Ameniuliza maswali mbalimbali kuhusu Yanga nimemweleza na akaniambia kama watamfuata na dau zuri ataweza kuja.

“Jesse ni mshambuliaji bora ambaye unaweza usimwone anasukumana uwanjani lakini ukamuona anashangilia mabao uwanjani.”

Advertisement