Mkimleta kaseja naondoka

“Kama wanaona nimeshindwa kuisaidia timu ni bora tukaachana salama tu, mkataba wangu umebaki miezi sita tu, bado kuna timu kibao zinanihitaji hivyo ni vyema tukamalizana mimi niende sehemu nyingine, siwezi kubali soka langu liishe mapema kiasi hicho.”

Muktasari:

Baada ya kuwepo kwa taarifa za Ivo kutemwa na Simba kwenye usajili wa dirisha dogo, klabu kadhaa zimeanza kumtolea macho kipa huyo zikiwemo Gor Mahia na KCB pia ya Kenya.

KIPA namba moja wa Simba, Ivo Mapunda, amewaambia viongozi wake kuwa kama watamsajili Juma Kaseja kisiasa yeye ataondoka.

Ivo aliweka wazi kwamba kamwe hatokubali kuingizwa kwenye siasa za viongozi wa klabu hiyo na kama wameona kuna tatizo katika kazi yake ni bora wakamalizana naye ili aende kutafuta riziki sehemu nyingine.

Ivo alisema anasikitishwa na taarifa zilizosambaa kuwa viongozi wa klabu hiyo wamepanga kumtema ndani ya usajili wa dirisha dogo bila sababu za msingi na akasisitiza kwamba kufanya vibaya kwa timu hiyo hakukuchangiwa hata kidogo na matatizo ya golikipa.

Akizungumzia taarifa za kusajiliwa kwa kipa Juma Kaseja, alisema hajaona umuhimu wa klabu yake kusajili kipa kwa wakati huu ambapo yeye na makipa wenzake, Peter Manyika Jr na Hussein Shariff ‘Casillas’ bado wameonyesha uwezo mzuri.

“Kwenye mechi zote za awali msimu huu hakuna matatizo tuliyopata ambayo unaweza kusema kuwa yalitokana na matatizo ya magolikipa moja kwa moja, tatizo ni kwamba mimi niliumia na mwenzangu Casillas naye aliumia, sidhani kama kuna haja ya kusajili kipa mpya,” alisema.

“Tatizo ninaliona hapo ni siasa za viongozi, wanataka kucheza mpira wa siasa ambao mimi siwezi kukubaliana nao, wataanza kusema huyu wetu huyu wao kitu ambacho hakipo, siasa hizi ndizo zilichangia mimi kufulia kipindi cha nyuma, siwezi kukubali zirudi tena.

“Kama wanaona nimeshindwa kuisaidia timu ni bora tukaachana salama tu, mkataba wangu umebaki miezi sita tu, bado kuna timu kibao zinanihitaji hivyo ni vyema tukamalizana mimi niende sehemu nyingine, siwezi kubali soka langu liishe mapema kiasi hicho.”

Ivo ni kipa mwenye uzoefu aliyewahi kucheza Yanga, Prisons, Moro United, St. George’s ya Ethiopia na Gor Mahia ya Kenya.

Baada ya kuwepo kwa taarifa za Ivo kutemwa na Simba kwenye usajili wa dirisha dogo, klabu kadhaa zimeanza kumtolea macho kipa huyo zikiwemo Gor Mahia na KCB pia ya Kenya. Ivo amewahi kucheza soka la kulipwa nchini Kenya kwa zaidi ya miaka mitatu akizidakia timu za Gor Mahia na Bandari FC.

Imeelezwa kwamba endapo Kaseja atatua Simba atasaini mkataba wa mwaka mmoja na si miaka miwili kama viongozi wa Simba walivyotarajia, ingawa bado hawajakubaliana kwa hilo.

Sababu kubwa za Kaseja kutaka mkataba wa mwaka mmoja ni baada ya kushauriwa kuwa aangalie kwanza kiwango chake kwani akiwa Yanga alikuwa hapati nafasi ya kucheza na pia kuangalia mwenendo wa Simba kwa mechi zijazo. Kaseja kupitia kwa meneja wake tayari ameiandikia Yanga barua ya kutaka kuvunja mkataba wake baada ya klabu hiyo kushindwa kummalizia fedha zake za usajili alizoahidiwa kupewa Januari mwaka huu pamoja na kutotekeleza baadhi ya mambo waliyokubaliana ikiwemo bima ya afya na kutopangwa kucheza.