Mkataba wa Morrison, Simba utata mtupu

Muktasari:

 Morrison amekuwa katika mgogoro na Yanga tangu alipoikacha klabu hiyo mwaka huu.

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amesisitiza kufuatilia kwa kina sakata la mkataba wa Bernard Morrison na Simba, ambao unalalamikiwa na Yanga kuwa una mapungufu.

Yanga waliibua upya sakata la winga huyo kwa kudai kuwa mkataba wake mpya alioingia na Simba hauna saini za kiongozi yeyote wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati Karia akisisitiza hivyo, Mwanasheria wa kujitegemea, Kasanda Mitungo alisema kama mkataba ulioonyeshwa na Yanga juzi ndiyo uliompa uhalali mchezaji huyo kucheza Simba, basi leseni yake ni batili.

Juzi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema wamepata mkataba wa Simba na Morrison.

Yanga na Morrison waliingia kwenye mgogoro wa kimkataba, ambapo Morrison aliishitaki Yanga kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji ya TFF akidai kwamba saini yake imeghushiwa.

Yanga walidai kuwa Morrison ni mchezaji wao kwani alisaini mkataba mpya wa miaka miwili, ambao mchezaji huyo aliukana.

Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji chini ya mwenyekiti wake, Elias Mwanjala ilitoa hukumu kwamba Morrison ni mchezaji huru ikidai mkataba wake na Yanga ulikuwa na mapungufu, na mchezaji huyo kujiunga na Simba siku chache baadaye.

Uongozi wa Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti, Mwakalebela ulidai kubaini mapungufu kwenye mkataba wa Simba na Morrison, jambo ambalo TFF inalifuatilia.

“Msimamo wa TFF ni ule ule, suala la Morrison kama tulivyosema tunalifuatilia na tukikamilisha tutalitolea tamko,” alisema Karia.

Akizungumza kisheria jana, Wakili Kasanda alisema pamoja na mkataba huo kuwahusu Simba na Morrison, Yanga ina haki ya kuulalamikia kwa kuwa ni mdau.

“Kama ni kweli, mkataba unaoonyeshwa na Yanga kuwa ndiyo uliompa uhalali Morrison kucheza Simba, kama ndiyo mkataba halisi, basi una mapungufu na leseni iliyotolewa kwa kutumia mkataba huo nayo ni batili,” alisema.

Licha ya mwanasheria na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Damas Ndumbaro kusisitiza kuwa wanaoweza kulalamika kwenye mkataba huo ni wale ambao ni sehemu ya mkataba na Yanga hawawezi kulalamika popote sababu si sehemu ya mkataba ule, Kasanda amekuwa tofauti akibainisha kwamba, Yanga ana nafasi ya kulalamika kama mdau kwenye ligi.

“Mkataba kama ni ule ambao Yanga wanadai ndiyo Morrison ameingia na Simba, basi utakwenda kuathiri hadi ligi, kwani klabu itakuwa imemtumia mchezaji ambaye usajili wake haujakamilika kwa kuwa mkataba ule unaonekana ni wa upande mmoja,” alisema.

Alisema cha msingi ni kujua uhalali wa mkataba ule ambao Yanga wameuonyesha kuwa ni wa Simba na Morrison kama ndiyo huo huo ambao huko TFF, kama ndivyo basi leseni iliyotolewa kwa kutumia mkataba ule ni batili.

Ingawa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwanjala alipoulizwa juu ya uhalali wa mkataba huo alisema yupo kijijini kwao Kyela na hana taarifa rasmi, aliahidi kulifuatilia litakapomfikia.

“Kama mkataba haujakamilika, leseni ilitokaje? Hivyo klabu nyingine zina haki ya kuhoji sababu zinaathirika kwa kukutana na mchezaji ambaye usajili wake haujakamilika, ikithibitika lazima hatua zichukuliwe,” alisema Kasanda.

Imeandaliwa na Imani Makongoro, Charity James na Mwanahiba Richard

Kwa taarifa zaidi kuhusu wanasheria wamesema nini kuhusu madudu ya mkataba huo, maswali 10 yenye utata yanayosubiri majibu TFF, soma gazeti la Mwanaspoti leo Oktoba 3, 2020.