Mkata umeme Simba yamkuta

KIUNGO mkata umeme wa Simba Queens, Joelle Bukuru raia wa Burundi ameanza kuonja joto ya jiwe baada ya kuanzia benchi katika mchezo mmoja wa Ligi ya Wanawake Bara, tofauti na ilivyozoeleka na amekuwa na uhakika wa namba kikosini hapo.

Nyota huyo panga pangua ndani ya Simba Queens amekuwa mhimili muhimu kwenye kikosi hicho akiwa ni miongoni mwa waliocheza michezo mingi na kuwa na uhakika wa namba mbele ya makocha watatu, Mussa Mgosi, Sebastian Nkoma na Charles Lukula.

Msimu uliopita kwenye Ligi Kuu, Joelle alianza katika michezo 20 kati ya 22 ya ligi, akikosekana kwenye mchezo mmoja dhidi ya Fountain Gate Princess ambao alikuwa majeruhi na mwingine dhidi ya Ilala Queens akianzia benchi.

Joelle alianza kikosi cha kwanza na kucheza dakika zote katika michezo yote miwili ya kirafiki kabla ya kuanza msimu mpya, mechi nne za ligi ya mabingwa Afrika Ukanda wa Afrika Mashariki na mechi tano za fainali za Ligi ya Mabingwa nchini Morocco.

Mrundi huyo hakuanza katika mchezo uliopita dhidi ya Amani Queens ya mkoani Lindi na timu yake iliibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 katika Uwanja wa Nyangao, Lindi.

Meneja wa Simba Queens, Seleman Makanya alisema nyota huyo kupumzishwa kwa mara ya kwanza ni mipango ya mwalimu kulingana na aina ya mchezo, huku akisisitiza ni mchezaji muhimu katika kikosi hicho.

Mmoja wa maofisa wa timu hiyo (jina tunalo), aliliambia Mwanaspoti kiungo huyo hana majeraha bali kocha aliamua kumpuzisha ili arudi kwenye kiwango chake baada ya kutumika mfululizo, huku akiwapa nafasi wengine ili anapokosekana isilete shida kwenye timu.

“Hana jeraha mwalimu kaamua kumpumzisha kidogo ili arudi ‘form’ unajua sasa hivi Joelle hachezi kama tunavyomjua kwa hiyo mwalimu anampa ‘break’ kidogo mechi ijayo atakuwepo Inshallah, si unajua yule anatumika sana.”

“Kuna mechi nyingine ambazo ana uhakika siyo ngumu anawapa nafasi wengine pia, ni wakati mzuri wa kupata mbadala wake wa ku ‘rotate’ japokuwa uwezo wake ni mkubwa na sasa hivi ligi imekuwa ngumu ushindani ni mkubwa,” alisema.