Mkao wa fainali: Afrika yaitabiria Simba maajabu

Muktasari:

  • KOCHA Mkongomani, Raoul Shungu bado ana maumivu ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka Simba na ametamka kwamba Wekundu hao wana uwezo mkubwa wa kucheza fainali na hao watakaokutana nao robo fainali wakae chonjo.

KOCHA Mkongomani, Raoul Shungu bado ana maumivu ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka Simba na ametamka kwamba Wekundu hao wana uwezo mkubwa wa kucheza fainali na hao watakaokutana nao robo fainali wakae chonjo.

Simba msimu huu imeipiga AS Vita inayofundishwa na kocha Mkuu Florent Ibenge akiwa na msaidizi wake Shungu nje ndani. Walipigwa bao 1-0 kisha wikiendi iliyopita wakachukua 4-1 na kutupwa nje hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Shungu ambaye ni Kocha wa zamani wa Yanga, alisema Simba wana timu bora ambayo iliwazidi ambapo katika kufuzu kwao kwenda robo fainali kama watakutana na timu laini basi watatua nusu fainali.

“Najua watakutana na timu za pili katika makundi mengine sasa hapo inategemea na uzuri wa timu watakayokutana nayo kama nao watakuwa na makosa kama tulivyofanya sisi wataingia hatua na nusu fainali,” alisema Shungu ambaye anazungumza kiswahili kizuri kwa lafudhi ya Kicongo.

“Unatakiwa uwe na timu yenye sura ya ubora kama wa Simba pia uwe na mpango mzuri wa kuwazuia,tulifanya makosa sana walitawala eneo la kati hili ni kosa ambalo kila nikilikumbuka naumia moyo,” alisema Shungu.

Shungu alisema anafahamu hatua ngumu zaidi kwa Simba itakuwa ni kuvuka kuanzia hatua ya nusu fainali lakini hata hapo watakaokutana nao wanatakiwa kujipanga kwani kosa kidogo wanaweza kuwaona Simba wanacheza fainali ingawa haitakuwa rahisi kwao.

“Nusu fainali wanaweza kufika na hapo itategemea pia watakutana na timu gani wakiwadharau kisha Simba kujipanga vizuri wanaweza kucheza fainali ingawa sio rahisi sana kucheza fainali.

“Hatua ya nusu fainali wanaweza kukutana na timu zilizoongoza makundi kama wao na hapo ndipo ugumu kwao utakuja lakini kwenye mpira lolote linaweza kutokea kwao.”

Tayari Simba imeondoka jana Jumanne na kikosi kamili kuelekea nchini Misri kucheza mchezo wa kukamilisha ratiba dhidi ya Al Ahly ambao nao wamefuzu wakimaliza nafasi ya pili katika kundi lao A ambalo linaongozwa na wekundu hao wa Msimbazi wenye pointi 13.