Miyeyusho afunguka ishu ya dawa za kusisimua misuli

Miyeyusho afunguka ishu ya dawa za kusisimua misuli

Muktasari:

  • Miyeyusho ni miongoni mwa mabondia wakongwe kwenye ndondi wanaoendelea kufanya vizuri mpaka sasa, ameanza ngumi Januari 1998 mpaka sasa amecheza mapambano 62 na kushinda mapambano 41.

Bondia Francis Miyeyusho ameijibu kambi ya Deo Samwel ambayo inadai ina wasiwasi bondia huyo kuwa anatumia  dawa za kusisimua misuli.

Miyeyusha amedai kuwa kambi ya Samwel imekuwa ikimshutumu kwamba huenda dawa hizo ndizo zimemsaidia kupata ushindi wa Technical Knock Out (TKO) usiku wa kuamkia leo.

Miyeyusho amemchapa Deo Samwel raundi ya nane na ya mwisho ya pambano hilo la dabi ya Dar es Salaam lililopigwa kwenye uwanja wa Kinesi, Urafiki.

Katika pambano hilo, Deo Samwel alijibu mashambulizi na mchezo kuwa wa piga nikupige hadi raundi ya saba, kabla ya bondia huyo anayetokea kambi ya Respect ya Manzese kushambuliwa bila majibu raundi ya nane na kuokolewa na refarii, Pembe Ndava.

Baada ya pambano hilo, kocha Christopher Mzazi anayemnoa Deo Samwel alisema ana wasiwasi mpinzani wao ametumia dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku michezoni, huku Miyeyusho akijibu mapigo na kusema kocha huyo ndiye itakuwa amempa bondia wake.

"Kama hawajatumia kwa nini wawe na wasiwasi, siku zote anayetumia dawa anakuwa na wasiwasi, wale walitamba kuwa watanipiga kwa Knock Out (KO), ila kilichowatokea wamekosa kisingizio na kujikuta wakizusha natumia dawa za kusimua misuli.

"Niko tayari kupimwa na wao waje tukapimwe ili tubaini nani anatumia dawa hizo, sijawahi na sifikirii kutumia dawa hizo katika maisha yangu ya ngumi, Deo Samwel nimemzidi ubora, uzoefu na hata maandalizi," amesisitiza Miyeyusho.

Kocha Mzazi alidai kwa nguvu alizokuwa nazo Miyeyusho na kuna raundi alishambuliwa lakini alibaki amesimama wanataka bondia huyo apimwe kama alitumia dawa ndipo watakubali ushindi wake.

"Narudia tena, sijawahi na sitarajii kama ipo siku itatokea, niko tayari hata sasa kupimwa, kambi ya Deo Samwel ikubali hainiwezi, isitafute visingizio visivyokuwa na sababu," ameongeza Miyeyusho.

...........................................

Na Imani Makongoro